Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
kwa kusimamia vyema utekelezaji wa masuala ya ajira kwa wazawa (Local Content),
hususan katika miradi mikubwa ya sekta ya nishati, ikiwemo Mradi wa Bomba la
Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo, tarehe 24 Machi 2025,
wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini walioitaka Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania wanapewa kipaumbele cha
ajira katika miradi ya kimkakati ya sekta ya nishati
Dkt.Biteko ameeleza kuwa, EWURA imekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha sera na miongozo ya ushiriki wa wazawa inatekelezwa kwa ufanisi,
jambo ambalo limewezesha wazawa kunufaika na fursa za ajira na zabuni katika
miradi mikubwa.
“EWURA imefanya kazi kubwa kuhakikisha watanzania
wananufaika na fursa zilizopo katika miradi ya kimkakati kama EACOP. Naipongeza
sana kwa kazi hii kubwa inayoendelea kufanya. Niwahakikishie kuwa Serikali
itaendelea kusimamia sera za ushiriki wa wazawa ili kuhakikisha kuwa rasilimali
za taifa zinawanufaisha wananchi wake,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na
wadau mbalimbali wa sekta ya nishati ili kuimarisha ushiriki wa wazawa katika
miradi yote inayoendelea na inayotarajiwa kuanza kutekelezwa nchini.
Post a Comment