HAYATI MAGUFULI ALIKUWA MSIMAMIZI WA RASLIMALI ZA NCHI - ASKOFU NIWEMUGIZI

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara,Severine Niwemugizi
......................

Na Daniel Limbe,Chato

WATANZANIA wamekumbushwa kuyaishi maisha mema ya aliyekuwa Rais wa Tanzania,Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alitanguliza uzalendo na kusimamia kwa moyo raslimali za taifa.

Aidha alionyesha unyenyekevu mkubwa mbele za Mungu na kutatua changamoto za makundi ya watu wanyonge ambayo yalionekana kuporwa haki kutokana na sababu mbalimbali.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, ameyasema hayo wakati akiongoza Ibada maalumu ya kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania,Dkt. Magufuli, huku akiwataka viongozi wa Umma kuyaiga mazuri yote aliyoyafanya enzi za uhai wake ili kudumisha amani na utulivu wa kitaifa.

Ibada hiyo imefanyika kwenye Kanisa la  Mtakatifu Yohana Mariamzeyi Parokia ya Mlimani Rubambangwe wilayani Chato mkoani Geita,na kuhudhuriwa na mamia ya watanzania kumwombea mema katika pumziko la kilele.

Kutokana na hali hiyo,Askofu Niwemugizi amewataka viongozi wa Umma kufanya kazi kwa weledi ili kuacha alama njema wakati wa uongozi wao badala ya kuwa na machukizo kwa jamii.

"Tuandike Kitabu chetu vizuri kingali bado tunaishi,maana watu wanataka waishi kwa amani na utulivu".

"Kadhalika tunapaswa kuishi kwa misingi ya kumtanguliza mbele Mungu kama Hayati Dkt. Magufuli alivyopenda kusema maneno ya Tumtangulize Mungu,pamoja na tumrudie Mungu"amesema Askofu Niwemugizi.

Amesema Kanisa linamkubuka sana Hayati Dkt. Magufuli kwa uthubutu wake,kumtanguliza Mungu na kuonyesha wazi moyo wa uzalendo wa kulinda raslimali za nchi.

Na kwamba msimamo wa Kanisa hilo nikuendelea kumwombea Hayati Magufuli kila mwaka pamoja na marehemu wengine ili Mwenyezi Mungu awasamehe katika madhaifu yao ya kibinadamu waliotenda kingali wakiwa hai.

Mbali na hilo,amewataka watanzania wote ambao kwa namna moja au nyingine walikwazwa na Hayati Magufuli,wamsamehe kwa sababu alikuwa mwanamdamu na hayupo tena hapa duniani.

"Dkt. Magufuli alikuwa mwanadamu, na kama kuna aliowatendea mabaya, kwa niaba yake naomba mumsamehe,na asiyemsamehe nasema huyo siyo mkristo" amesema Askofu Niwemugizi.

Akitoa salaam za serikali kwa na niaba ya Rais Samia Suluhu, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu, William Lukuvi,amemshukuru sana Askofu Niwemugizi kwa kuwakumbusha viongozi wa umma kufuata misingi ya uzalendo na utawala bora.

Aidha amesema Rais Samia anaungana na familia ya Hayati Magufuli pamoja na watanzania wote katika kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha Hayati Dkt. Magufuli na kwamba ni kiongozi aliyefanya naye kazi kwa ukaribu zaidi akiwa msaidizi wake kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia amemshukuru kwa maombezi na dua kwa viongozi walioko madarakani na kwamba serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza miradi yote iliyoachwa na Hayati Dkt. Magufuli.

Baadhi ya viongozi wengine walioshiriki Ibada ya Misa ya kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha Hayati Dkt. Magufuli,ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa,Makamu mwenyekiti UVCCM taifa,Rehema Sombi, Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicolaus Kasendamila na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Luhumbi.

Rais Dkt. Magufuli, alifariki dunia Machi 17, 2021 wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo kwenye hospitali ya Mzena iliyopo Jijini Dar es salaam.

                         Mwisho.



0/Post a Comment/Comments