MAAMBUKIZI YA ZINAA NA VVU YAPAA BIHARAMULO

Diwani viti maalumu kata ya Nyakahura Ziyun
 Hussein,akiwasilisha taarifa ya Kata kwenye kikao cha Baraza la madiwani
..........

Na Daniel Limbe, Biharamulo.

MWINGILIANO mkubwa wa watu, kutojali taratibu na kanuni za kufanya ngono salama, na umaskini wa vipato umedaiwa kuchochea maambukizi mapya ya magonjwa ya zinaa na virusi vya ukimwi kwa wananchi wa kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Hatua hiyo inatishia jitihada za idara ya afya za kupambana na maambukizi mapya ya magonjwa hayo,kutokana na jamii kutojali madhara yanayoweza kutokea siku za usoni na kwamba hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kunusuru ongezeko hilo ambalo ni tishio kwa ustawi wa taifa.

Katika taarifa ya kata ya Nyakahura iliyowasilishwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, inaonyesha kuwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba 2024, Magonjwa ya zinaa yameongezeka baada ya watu nane kubainika kuambukizwa.

Taarifa hizo ni kutokana na jitihada za wataalamu wa afya kufanya vipimo mbalimbali kwa wananchi waliokwensa kupata huduma za afya katani humo.

Aidha takribani wananchi 36 wamebainika kuambukizwa virus vya ukimwi(VVU) kwa kipindi hicho licha ya jitihada za serikali kuendelea kuelimisha jamii kuzingatia mapenzi ya ngono salama.

Diwani viti maalumu kata ya Nyakahura Ziyun Hussein,amesema ongezeko hilo linachangiwa na uwepo wa kundi kubwa la vijana wanaotekeleza mradi ya ujenzi wa barabara ya lami ya Rusahunga kwenda Rusumo wilayani Ngara, pamoja na maegesho makubwa ya magari yanayo toka ndani na nje ya nchi.

Aidha amesema jitihada za kutolewa elimu kwa jamii kutambua uwepo wa ongezeko la maambukizi hayo zinapaswa kuchukuliwa haraka ili watu wachukue tahadhali badala ya kuendelea kuwa siri kwa wataalam wa afya na waathirika pekee.

Kutokana na hali hiyo,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, ameonyesha kushangazwa na mlipuko wa magonjwa hayo licha ya uwepo wa watu zaidi ya 600 wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi(ARVs) kwenye kata hiyo.

"Kwa mujibu wa taarifa ya kata ya Nyakahura inaonyesha kuna ongezeko kubwa la magonjwa ya zinaa ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu pekee watu nane wameambukizwa magonjwa hayo,na hiyo ni kwa wale waliokwenda kupata huduma za afya,hali hii inatisha na tunapaswa kuchukua hatua za haraka kuelimisha jamii hiyo"amesema Rushahu.

Ikumbukwe kuwa serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kudhibiti magonjwa ya zinaa na VVU katika jamii,huku baadhi ya nchi wafadhili wa dawa hizo wakiwa wametishia kusitisha utoaji wa dawa na fedha za mapambano ya udhibiti wa ugonjwa wa Ukimwi, hasa kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Mwisho.

0/Post a Comment/Comments