"Tenda wema nenda zako" ndiyo unavyoweza kusema kutokana na semi zilizowahi kunenwa na wahenga, wakimaanisha siyo kila jambo jema unalomtendea mtu lazima upate malipo ya wema huo wakati huo.
Kauli hiyo ndiyo iliyomsukuma Diwani wa viti maalumu kata ya Nyakahura(CCM) Ziyun Hussein,ambaye amejitolea kuishi na watoto wawili waliotelekezwa na mlemavu wa akili muda mfupi baada ya kujifungua kwa kutumia pesa anayopata kupitia posho ya udiwani wake.
Watoto hao walizaliwa baada ya mama mwenye ulemavu wa akili kubebeshwa mimba kwa nyakati tofauti na watu wasiojulikana kabla ya diwani huyo kuchukua uamuzi wa kuwalea kutokana na mama yao mzazi kuwa na tabia ya kujifungua na kuwatelekeza pasipo kuwahudumia mahitaji muhimu kwaajili ya makuzi yao.
"Baada ya mtoto wa kwanza kuzaliwa kwenye pagala la nyumba, mama yake aliondoka naye na kwenda kumtelekeza pembezoni mwa bwawa la kuchota maji, na baada ya wananchi kuona mtoto akilia pasipo msaada walinipigia simu nikaenda kushuhudia na kuchukua uamuzi wa kumlea mtoto huyo"amesema Ziyun.
Diwani huyo ameiambia Torch Media kuwa baada ya mwaka mmoja mwanamke huyo alibebeshwa mimba nyingine na mtu asiyejulikana,baada ya kujifungua alimtelekeza tena mwanaye huyo, ndipo diwani huyo akalazimika kumchukua dhamana ya kuishi na watoto hao, huku akisema matunzo yote ya watoto hao yanatokana na posho yake ya udiwani.
Mwisho.
Post a Comment