*****
Na Daniel Limbe,Biharamulo
MKUU wa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, ACP. Advera Bulimba,amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kupunguza hofu ya kutolewa kwenye nafasi zao katika Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani mwaka 2025 kwa madai kwamba kazi walizofanya kwenye kata zao zimetukuka.
"Niwatake madiwani mtulie kwenye kata zenu vizuri,msiwaogope wanaojipitisha muda utakapofika na kipenga kikapulizwa inabidi muingie uwanjani kupambana, maadamu naamini hata ninyi kuvaa jezi vizuri mnaweza" amesema.
Alikuwa akitoa salaamu za serikali kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,ambapo pamoja na mambo mengine amewataka madiwani hao kutembea kifua mbele kutokana na utekelezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
Aidha amewataka kuyasema mema yote yaliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ametoa zaidi ya shilingi bilioni 94.7 za maendeleo kwenye sekta mbalimbali zilizopo kwenye wilaya hiyo.
Aidha amempongeza Diwani wa kata ya Ruziba,Athanase Sumbuso, kutokana na jitihada zake za kutoa taarifa haraka kwa mkuu wa wilaya hiyo baada ya kutokea vifo vya watu nane wa familia moja ambao awali walihofiwa kufa kutokana na imani za kishirikina kabla ya serikali kufanya uchunguzi wa kifo cha Mchungaji wa Kanisa la Ebeneza, Erasto Kagenzi,ambaye alikuwa akitoa huduma za maombezi kwenye familia hiyo.
"Nitumie fursa hii kumpongeza sana Diwani wa kata ya Ruziba,kwa kuamua kutoa taarifa za haraka kwangu baada ya kuona vifo visivyokuwa vya kawaida kwenye kata yake,fikiria kama asingetoa taarifa hali ingekuwaje kule"amehoji Bulimba.
Awali Muuguzi mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Revocatus Salala,akiongea kwa niaba ya Mganga mkuu wa wilaya hiyo,amesema serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Marburg, na kwamba tangu Novemba 20,2024 baada ya rais Samia kutangaza rasmi uwepo wa ugonjwa huo nchini,ni wagonjwa wawili pekee ndiyo waliokufa mpaka sasa.
Post a Comment