Mwakilishi wa mgeni rasmi akitoa nasaha kwa wananchi pamoja na wachezaji
Kaimu Mkurugenzi Chawassa, Magreth Protas(katikati),akitoa nasaha mbalimbali


Timu ya Muungano FC(jezi bluu) ikisalimiana na Usalama FC (jezi nyeupe) katika fainali ya Chawassa maji Cup.
.........,
Na Daniel Limbe, Chato
TIMU ya mpira wa miguu ya Muungano FC imeibuka mshindi wa mashindano ya Chawassa maji Cup 2025,baada ya kuifunga timu ya Usalama FC,iliyokuwa ikidhaminiwa na Jeshi la polisi wilayani Chato mkoani Geita.
Ushindi wa timu ya Muungano FC umepatikana dakika ya 71 ya mchezo huo baada ya mkwaju mkali wa Rubale Magesa, ambao ulimshinda mlinda mlango wa timu ya Usalama FC na hatimaye kuzama langoni, ambapo bao hilo limedumu hadi kipenga cha mwisho cha mwamuzi kilipopulizwa kuashiria kumalizika kwa mchezo huo.
Matokeo hayo yameisaidia timu ya Muungano FC kutwaa zawadi za mshindi wa kwanza ikiwemo Mbuzi wawili,huku mshindi wa pili Usalama FC ikijinyakulia Mbuzi mmoja na timu ya Kurugenzi FC, ikitwaa zawadi ya mshindi wa tatu ambayo ni shilingi 50,000.
Zawadi zingine za fedha zimekwenda kwa Kipa bora waashindano hayo, mchezaji bora na mfungaji bora.
Katika mashindano hayo yaliyo andaliwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chato(Chawassa) yalizikutanisha jumla ya timu nane huku timu nne zikiwa nimeundwa kutoka taasisi za Umma na nne kutoka kwenye jamii ya watumia maji katika wilaya ya Chato.
Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Mratibu wa mashindano hayo, Dickson Medard, amesema mashindano hayo yametumika kuhamasisha jamii kulinda na kutunza miundo mbinu ya maji, kutatua kero za watumia maji na kujibu maswali mbalimbali yahusuyo upatikanaji wa maji safi na salama katika jamii.
Aidha Mamlaka hiyo imetumia fursa hiyo kutoa msamaha kwa wateja waliokuwa wamekatiwa huduma ya maji kutokana na madeni,ambapo wamerudishiwa huduma kwa makubaliano ya kulipa taratibu(kidogo kidogo) ikiwa ni kutii maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kadhalika mashindano hayo yametumika kutangaza unafuu wa kuvuta maji kwa jamii ikiwa ni kuadhimisha wiki ya maji kitaifa ambapo wananchi wa wilaya ya Chato waliondani ya mita 60 ya linapopita bomba kuu watanufaika na huduma ya kuvuta maji majumbani mwao kwa gharama ya shilingi 180,000 badala ya Sh. 300,000 zinazotakiwa kutozwa.
Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chato, Magreth Protas, amezipongeza timu zote shindani katika mashindano hayo na kuhimiza kuzingatiwa kwa kauli mbinu ya wiki ya maji ambayo ni "Maji ni Uhai,maji ni Uchumi".
"Niwapongeze sana kwa ushiriki wa mashindano hayo binafsi naona yamefana sana,niwapongeze sana washindi mliofanikiwa kutwaa nafasi ya kwanza,bila kuwasahau waamuzi kwa kuchezesha fainali hii kwa haki,kikubwa zaidi tutambue kuwa maji ni Uhai na maji ni Uchumi kwahiyo tutunze miundo mbinu ya maji kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo" amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Louis Bura, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi wa mashindano hayo, Alexander Msisiri, amedai kufurahishwa na vipaji vingi vilivyoibuliwa katika mashindano hayo na kwamba hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira na uchumi wa vijana kupitia michezo.
Hata hivyo,amezitaka taasisi zingine za Umma kuiga mfano ulioonyeshwa na Chawassa,katika kudhamini mashindano mbalimbali kwa kuwa hali hiyo inasaidia kuimarisha uhusiano na jamii,kuwa na jamii yenye afya bora pamoja na kuongeza ajira kupitia michezo mbalimbali.
Aidha kupitia mashindano hayo,baadhi ya vijana waliofanya vizuri wataungana na wenzao waliopatikana kwenye mashindano ya Chato Samia Cup kutengeneza timu ya wilaya itakayo kwenda kushindana na timu ya wilaya ya Geita,katika kilele cha wiki ya maji ngazi ya mkoa hivi karibuni.
Baadhi ya timu zilizoshiriki katika mashindano hayo ni Usalama FC,Kurugenzi FC,Elimu FC,Chawassa FC, Rungwe City, Muungano FC, Kigongo Academy na Mbuye FC.
Mwisho.
Post a Comment