Serikali imeipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania –TMA kutokana na kazi inayofanya ya utoaji wa huduma za hali ya Hewa zilizoboreshwa ikiwa ni pamoja na utoaji wa tahadhari wakati wa matukio ya hali mbali mbaya ya hewa.
Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile wakati akiwasilisha ujumbe wa Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa katika katika maadhimisho ya hali ya hewa Duniani ambayo hufanyika machi 23 kila mwaka ambapo imekwenda sambamba na kaulimbiu isemayo ‘Kwa pamoja tushughulikie pengo la utoaji wa tahadhari’.
Amesema kuwa Tanzania kama mwanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani na Umoja wa Mataifa imechukua hatua kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na mapungufu katika utoaji wa tahadhari kwa kufanya uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa.
Naibu Waziri Kihenzile amesema kuwa serikali itaendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa zaidi na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Mamlaka hiyo.
Aidha kuhusu ustahimilivu na kupunguza athari za mabadiliko y ahali ya hewa na tabia nchi amesema serikali imeweka na inatekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania –TMA,Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa jopo la KImataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dkt Ladislaus Chang’a amesema juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali zimesababisha kuongezeka kwa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hadi kufikia zaidi ya asilimia 88% kwa sasa.
Post a Comment