Na Daniel Limbe,Chato
BARAZA kuu la waislamu Tanzania (Bakwata) wilayani Chato mkoani Geita, limemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kuridhia ombi la kumalizia ujenzi wa msikiti mkubwa wenye uwezo wa kuchukua waumini 900 ambao ulikwama baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania,Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Uamuzi huo wa Rais Samia umepokelewa kwa shangwe kubwa baada ya baadhi ya waumini wa dini hiyo kupoteza matumaini ya ujenzi huo ambao umesimama kwa takribani miaka minne pasipo kujua hatma yake.
Akizungumza katika Ibada ya Ijumaa iliyofanyika kwenye msikiti wa wilaya hiyo, Shekhe wa wilaya ya Chato, Abdulrahiman Ismail,amesema alfajili ya leo amepokea ujumbe kutoka Ofisi ya Rais Samia ukimjulisha kuwa serikali imekubali kumalizia ujenzi huo.
Kutokana na hali hiyo, Shekhe Abdulrahiman ametumia fursa hiyo kuwatangazia waumini wa dini hiyo na kumpongeza rais Samia kutengua kitendawili hicho ambacho kilikuwa kinaumiza nafsi za waislamu wengi kutokana na fedha nyingi zilizowekezwa katika ujenzi huo ambao ulikuwa ukisimamiwa na taasisi ya Al-Hiqma Foundation.
"Naomba nitumie nafasi hii kumtakia kila lillilo jema rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,mama yetu kipenzi Samia Suluhu Hassan,kwa kutukubalia maombi yetu ya kumalizia ujenzi wa msikiti wetu ambao ulianza kujengwa na mtangulizi wake aliyekuwa rais wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli".
"Mwenyezi Mungu amjalie kutimiza maono ya mtangulizi wake pamoja na mema wengine ambayo anakusudia kuyatekeleza kwaajili ya watanzania, tunayo Imani kubwa na Rais wetu kutokana na mambo makubwa anayoendelea kuyafanya kwa jamii na taasisi mbalimbali za dini" amesema Shekhe Abdulrahiman.
Khamis Issa(Burebure) amesema kitendo cha Rais Samia,kukubali kumalizia ujenzi huo ni cha kiungwana na kwamba anaye weza kumlipa swawabu hizo ni Mwenyezi Mungu pekee kutokana na hekma thabiti za kumjengea nyumba ya kuabudia waja wake.
Husna Hussein, amemtakia maisha marefu rais Samia katika uongozi wake na kwamba waumini wa dini hiyo wamepokea kwa mikono miwili uamuzi wa ukamilishwaji wa nyumba ya ibada uliokuwa umekwama miaka minne iliyopita.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mkuyuni ulipo msikiti huo,Goodluck Phinias,mbali na kumpongeza rais kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo kauli yake ya kuwa miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. Magufuli kuwa ataitekekeza,amesema uamuzi wa kumalizia ujenzi wa msikiti huo ni mapenzi ya dhati kwa wananchi wa wilaya ya Chato mkoani Geita,
"Naamini kukamilika kwa msikiti huo utaimalisha maadili katika jamii maana eneo hilo litasaidia waumini wa dini ya kiislamu kupata maelekezo na maonyo ya Mwenyezi Mungu hatua itakayosaidia kuimarisha amani,upendo na mshikamano ndani ya jamii" amesema Phinias.
Amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kusaidia ujenzi wa makanisa na misikiti maeneo mbalimbali ya nchi na kwamba jamii isiyokuwa na maadili ya Mwenyezi Mungu haiwezi kuishi kwa Usalama na amani.
Jengo la Msikiti lililokwama kukamilika kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
KONGOLE, MH LITAPITA LIMBE UMETUHESHIMISHA
ReplyDeletePost a Comment