SERIKALI YAWAONYA WATUMISHI MIUNGU WATU

Katibu tawala wilaya ya Chato,Thomas Dimme,akizungumza na watumishi wa Umma.

********

Na Daniel Limbe,Chato

SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imewaonya baadhi ya viongozi wa taasisi na wakuu wa idara za serikali kuacha kujigeuza Miungu watu, badala yake wafanye kazi na watumishi walio chini yao kwa ushirikiano na upendo hali itakayongeza ufanisi na kupunguza msongo wa mawazo kazini.

"Kukosekana kwa ushirikiano na kuwekeana matabaka ya kitaasisi ni chanzo cha kuporomoka uwajibikaji kazini,badala yake tunapaswa kuwa pamoja kama watumishi wa umma bila kujali,wewe ni askari Magereza,Polisi, JWTZ,Tanapa,Daktari,Nesi,mtumishi wa halmashauri wala mtumishi kutoka Ofisi wa mkuu wa wilaya".

Hayo yamesemwa na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Thomas Dimme,kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma yaliyofanyika kwenye viwanja vya VETA Chato baada ya kutanguliwa na michezo mbalimbali iliyofanyika kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa "Magufuli Studium".

Pomoja na mambo mengine,Dimme amepongeza jitihada za ujenzi wa uwanja wa Magufuli Studium ambao unatarajiwa kupokea timu mbalimbali za ligi kuu na daraja la kwanza kwaajili ya mazoezi ya soka,huku akiwataka wakuu wa taasisi kutoa fursa kwa watumishi wao kufanya michezo mbalimbali kwa lengo la kuimalisha afya zao.

"Tukumbuke kuwa michezo ni afya na pia ni ajira,tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi kila mara,hatua hiyo itaimalisha miili yetu kuepukana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ikiwemo kupunguza msongo wa mawazo"amesema Dimme.

Amedai kuwa maadhimisho hayo yamekusudia kuwaweka pamoja watumishi wa umma,kushirikiana, kupendana,kuthaminiana, kuhamasisha amani na maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla, na kwamba ni wajibu wa kila mtumishi kutimiza majukumu yake kikamilifu pasipo kuwa na uoga wa aina yoyote.

Miongoni mwa mambo yaliyotekelezwa katika maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ni pamoja na kupanda miti 2,000 kwaajili ya kuhifadhi mazingira kwa lengo la kuhifadhi uoto wa asili, kulinda uhai wa viumbe hai pamoja na uhakika wa kupata mazao ya miti siku za usoni.

Mkakati huo unaungwa mkono na nukuu ya mwana falsafa Chinese Proverb aliyesema "Muda mzuri wa kupanda mti ni miaka 20 iliyopita, Lakini muda mwingine mzuri wa pili ni sasa.”

Kadhalika baadhi ya wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali ya wilaya ya Chato,wamesaidiwa vifaa mbalimbali ikiwemo,sabuni,mafuta,miswaki pamoja na taulo za watoto.

Aidha baadhi ya watumishi wamefanikiwa kutembelea hifadhi ya kisiwa cha Rubondo ili kuhamasisha jamii kutembelea vivutio vilivyopo ndani na nje ya wilaya hiyo,hatua itakayosaidia kukuza pato la taifa.

    




0/Post a Comment/Comments