*****
Na: Hussein Chimba, Dodoma
Zama za kuhitaji watu wenye elimu ya makaratasi bila ujuzi, zimepitwa. Hivi ndivyo unavyoweza kusema katika suala zima la mahitaji ya raslimaliwatu katika kuajiriwa na kujiajiri pia. Watu wenye ujuzi wana uwanja mkubwa wa kuwa na uhakika wa kipato iwe kwa kuajiriwa au kujiajiri.
Pamoja na kwamba, kabla ya maboresho ya mtaala wa elimu hapa nchini, elimu yetu haikuweka mkazo katika ujuzi, lakini sasa yamefanyika maboresho makubwa ya mtaala wa elimu kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu ya mkondo wa jumla na mkondo wa amali (elimu ufundi) pia.
Kumekuwa na dhana potofu dhidi ya elimu ya ufundi kwa kudhani elimu ya ufundi ni kwa watu waliofeli. Hapana. Haiko hivyo. Dhana hii potofu imepelekea baadhi ya watu kubeza elimu ya ufundi huku wengi wakidhani ili kufanikiwa ni lazima wafike vyuo vikuu ili watunukiwe shahada. Jambo la kuzingatia ni kuwa, mahitaji ya sasa ni watu wenye ujuzi kwani ni ujuzi huo ndiyo utakaomuweka mhusika katika mazingira mazuri ya kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe.
Mjadala umekuwa mkubwa hasa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa rai kwa wahitimu wa vyuo vikuu wenye elimu ya Shahada kusoma kozi mbalimbali za ufundi katika vyuo vya ufundi kama vile Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ( VETA) ili kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na hivyo kuwa na kipato cha uhakika.
Baadhi ya watu wameunga mkono ushauri huo, huku baadhi wakibeza ushauri huo kwa kudhani wahitimu wa vyuo vikuu kwenda vyuo vya VETA ni uwashusha hadhi. Hapana. Katika zama hizi za changamoto za kupata ajira rasmi au raslimaliwatu wenye ujuzi, wahitimu wa vyuo vya ufundi wana nafasi kubwa. Hakuna haja ya kubeza VETA, twendeni VETA, kupata ujuzi utakaokuwa msaada wa kujikomboa kiuchumi na kuwa na kipato. Ahsante sana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa kutufumbua macho kuona fursa nzuri VETA.
Mwandishi wa Makala hii ni Mwalimu kwa Taaluma na Mchambuzi wa Masuala ya Elimu, Uongozi na Siasa.
Kwa maoni na ushauri, anapatikana kwa namba: 0764091917.
Post a Comment