Vijana nchini wamehimizwa kutunza mazingira ili kulisaidia Taifa kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira la WWF, Yohana Mpagama, wakati wa uzinduzi wa mpango wa kushirikisha vijana katika uhifadhi wa mazingira (WWF Youth Conversation Champion).
Mpagama amesema vijana ni nguvu kazi ya Taifa na wanahitajika katika kulinda mazingira.
"Nawapa rai vijana kuwa si nguvu kazi ya kesho, bali ni nguvu kazi ya leo. Mtambue wajibu wenu kama mabalozi wa uhifadhi wa mazingira ili kutimiza malengo yetu ya kuwa na dunia salama," amesema Mpagama.
Mpagama amesisitiza kuwa Shirika la WWF litaendelea kuwasapoti vijana katika kutunza mazingira na kusaidia kuondoa athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa WWF Tanzania, Joan Itanisa, amesema mpango huo wa kuwashirikisha vijana katika mazingira umewashirikisha vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini kwa lengo la kufikisha ujumbe kwenye maeneo wanayotoka na kuhamasisha vijana wenzao kuhusu kuhifadhi mazingira.
"Tumeona vijana hawashiriki kikamilifu katika kuhifadhi mazingira kwa kuona hakuna faida kwao na wengi wamejikita katika shughuli za kujitafutia kipato," amesema Joan.
Hata hivyo, Joan amesema uelewa bado ni kikwazo kwa vijana kuhusu uhifadhi, na kwamba WWF itaendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu uhifadhi.
Kwa upande wao, vijana walioshiriki katika mafunzo hayo ya siku mbili, akiwemo Joseph Magele kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi nchini, wamesema mpango huo umewajenga kuwa mabalozi wazuri katika utunzaji mazingira.
Amesema kwa sasa kuna ongezeko la joto ambalo limetokana na shughuli za kibinadamu.
Post a Comment