JKI YATOA MAFUNZO KWA WANAWAKE ATHARI ZA MIKOPO YA 'KAUSHA DAMU'


               ::::::::

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Jamii Kwanza Initiative(JKI) kwa Kushirikiana na Ofisiya Serikali ya Mtaa wa Amani Leo April 29,2025 imetoa mafunzo kwa wanawake kuhusu athari ya mikopo kandamizi (kausha damu) ili kuwawezesha kuepukana na adha na udhalilishaji wanaoupata wanapodaiwa.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo ambayo yamefanyika kata ya Kipunguni,Wilaya ya Ilala Jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa (JkI) Daniel Joseph Migera amesema kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo ili kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi.

"Wanawake wanapata changamoto na shida ambazo zinawafanya wakachukue mkopo ili waweze kuzitatua lakini badala ya wanaangukia kwenye mikopo ambayo inakuwa si yenye faida kwao" Amesema Migera 

Amesema kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mipango ya kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ya asilimia kumi ,hivyo kwa mafunzo wanayoyatoa watapata Elimu ya Fedha ambayo itawasaidia kwenye biashara zao.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Kipunguni Gamaliel Mhanga ameishukuru na kuipongeza Taasisi ya JKI na Mwenyekiti wa mtaa huo kwa kutoa mafunzo hayo kwani jambo hilo ni zuri na lipo kwenye ilani ya CCM ambayo inatekelezwa bila ubaguzi kwa Wananchi. 

Ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na CCM inahakikisha Wananchi wake wanakuwa na maisha nafuu na kazi ya viongozi ni kusimamia utekelezaji.

Ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kusikiliza kwa makini ,kuuliza maswali pale ambapo hawajaelewa ili baadae waweze kuyafanyia kazi.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani ,Abdi Mahanyu amesema kuwa lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuwa Fanya wanawake kuwa na maisha Bora na kuepukana na mikopo kandamizi(kausha damu).

"Leo tumeanza mafunzo haya kwa takribani wanawake 150, tutawafunza ili kuvunja minyororo ya mikopo isiyo na tija" Amesema Mahanya.

Nae Mmoja wa Washiriki, Mkuu Ramadhani amesema mafunzo hayo yamewaonyesha mwanga kwani kabla ya kupewa mafunzo yatawawezesha kufanya biashara bila kutegemea mikopo kandamizi(kausha damu).











0/Post a Comment/Comments