Na Daniel Limbe,Chato
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohammed Alli Kawaida, ameipongeza serikali kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji safi na salama utakao kuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 100,000 kwenye wilaya ya Chato mkoani Geita.
Mradi huo ambao ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwenye miji 28 nchini, unatarajiwa kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji safi na salama, ambapo kwa sasa baadhi yao wanalazimika kutumia maji yasiyo salama kutoka ziwa Viktoria ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Chato kwenye kijiji cha Buzirayombo mkoani humo wakati akikagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika sekta ya maji, Kawaida amesema Chama hicho kinaridhishwa na serikali ya awamu ya sita,chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, jinsi inavyoendelea kutekeleza azma yake ya kumtua mama ndoo kichwani.
Amesema Chama hicho kitaendelea kuisimamia serikali ili kuhakikisha miradi ya maji inaendelea kujengwa maeneo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha hiyo, na kwamba hawana budi kuendelea kukiamini chama hicho kwa madai ndiyo pekee kinachoweza kutatua changamoto za jamii.
Mbali na pongezi hizo, kawaida amelazimika kufikisha salamu za Rais Samia kwa wananchi wa wilaya hiyo,kwa madai kuwa Chato ni nyumbani kwao kwa mara ya pili kutokana na ukweli kwamba mtoto wa Chato ambaye ni Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli,ndiye aliyemuibua kufikia nafasi aliyonayo baada ya kumuamini na kumpa nafasi ya kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo, Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chato(Chawassa) Mhandisi Isack Mgeni,amesema mradi huo umefikia aslimia 49 na kwamba unatarajiwa kukamilika kwa aslimia 100 ifikapo Desemba 2025.
Aidha kwa awamu ya kwanza mradi huo utatekelezwa katika kata sita za wilaya ya Chato na kwamba upanuzi wake utaendelea kulingana na mahitaji ya Umma na uwezo wa mradi huo ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 38.
Hata hivyo,amesema miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mradi huo ni pamoja na wale wasiojiweza pamoja na wanaozunguka chanzo cha mradi huo ambapo takribani wananchi 500 watavutiwa huduma ya maji ya bomba majumbani mwao bure.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Buzirayombo,akiwemo Jawabu Abduli na Faustine Ernest wameipongeza serikali kwa kuweka chanzo cha mradi huo kwenye kijiji chao na kwamba hatua hiyo imewasaidia kupata ajira za muda mfupi na kuboresha maisha yao ukilinganisha awali kabla ya ujio wa mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Peter Bura, amemshukuru Rais Samia kwa utayali na mapenzi yake mema kwa wananchi wa wilaya hiyo,kwa kuamua mradi mkubwa wa maji kujengwa Chato, na kwamba kukamilika kwake utasaidia sana uchumi wa kaya, wilaya,mkoa na taifa kwa ujumla.
Kadhalika amewapongeza wananchi wa kata ya Bukome kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa kwa serikali katika kuimalisha ulinzi wa miundombinu ya ujenzi tangu mwanzo wa mradi hadi sasa, na kwamba hakuna madai yoyote ya upotevu wa vifaa kwa wakandarasi.
Post a Comment