MALIASILI SC YATIKISA SINGIDA.


...,..........

Na Sixmund Begashe 

Club ya Michezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama MNRT SPORTS CLUB imeibua gumzo la shangwe Mkoani Singida kwenye mashindano ya Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani MEI MOSI 2025, Mkoani Singida, kutokana ushujaa wa timu zake hususani timu ya mchezo wa kuvuta kamba wanaume iliyofanya vizuri mpaka mwisho.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Singida na viunga vyake wamesikika wakiwapongeza wachezaji wa timu za Club hiyo yenye wachezaji wenye mbinu na ujuzi mkubwa, kwa kupambana vikali kwenye michuano hiyo hali inayoleta hamasa ya watu kupenda michezo na burudani ya aina yake.

Akizungumza na Maliasili Media, Bi. Mwantum Shabani wa Manyoni Singida amesema japo timu ya Maliasili Sports Club Wanaume Kamba imeshika nafasi ya pili lakini imeonesha upinzani mkali dhidi ya timu zingine pinzani.

" Singida kama burudani tumepata, mimi timu yangu ilikuwa Maliasili, si kwa sababu tu wanatulindia Maliasili zetu na kutuletea mapato kupitia Utalii, pia kwa namna walivyojipanga kwenye michezo hii, yaani ukishangilia hii timu haikuangushi, najivunia kuona wameibuka na Kombe hili naamini mwakani watakuwa washindi wa kwanza". Aliongeza Bi. Shabani.

Akizungumzia mashindano hayo makubwa hapa nchini, Mwenyekiti wa MNRT SPORTS CLUB Bw. Gervas Mwashimaha ameushukuru uongozi wa Wizara hiyo kwa kuiunga mkono club hiyo hali iliyowatia moyo na hari kubwa Kipindi chote cha michuano hiyo na kuahidi kuendelea kufanya vyema zaidi katika michezo mingine watakayo shiriki.

Katika mchezo wa Fainali wa Kamba wanaume, timu ya Maliasili imeshika nafasi ya pili dhidi ya timu 47 zilizoshiriki mashindano hayo huku timu ya Uchukuzi wanaume Kamba ikishika nafasi ya kwanza.

0/Post a Comment/Comments