MBUNGE BALOZI MULAMULA - TUUENZI NA KUUDUMISHA MUUNGANO NIWAPEKEE AFRIKA


*******

MBUNGE Balozi Liberata Mulamula, amesisitiza Watanzania kuendelea kuuenzi na kuudumisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao umekuwa na tija kubwa nchini huku ukiwa ni wa mfano wa kuigwa Afrika kwa kudumu miongo sita ukiwa imara.

Balozi Mulamula ameyasema hayo wakati akielezea tija ya Muungano huo, ikiwa ni siku chache kuelekea kilele cha maadhimisho ya Muungano huo, ambayo hufanyika Aprili 26 kila mwaka.

"Tunaposheherekea miaka 61 ya Muungano wetu ni vyema kuwashukuru waasisi wetu, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume, kwa maono yao ya mbali kuanzisha muungano katika juhudi za kujenga mustakabali wa Taifa letu kwa misingi ya umoja, amani na usalama.

"Sisi tuliozaliwa kabla ya muungano, tumeuishi muungano, tumetumikia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tumeona faida za utaifa wetu," alisema.

Alisema Tanzania inajivunia katika Bara la Afrika kuwa ni Muungano pekee uliodumu miongo sita hadi sasa na unaendelea kuimarika licha ya kero kadhaa zilizojitokeza katika historia ya Muungano huo.

Alisema kero hizo zinashughulikiwa kupitia njia ya majadiliano na maridhiano ya pande zote mbili za serikali ya Muungano, kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwamba Ili nchi iendelee inahitaji mambo matatu: Watu, Siasa Safi na Uongozi Bora.

"Falsafa hii ndiyo, imedumisha Muungano wetu. Tumekuwa na Viongozi bora katika awamu zote ambao wamelinda na kudumisha Muungano wetu kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake, Tunakoelekea ni pazuri. Yaani ‘Kazi na utu tunasonga mbele,"alisema.

Alisisitiza kuendelea kuuenzi na kuulinda muungano kwa kuwaunga mkono viongozi wa serikali Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

0/Post a Comment/Comments