"""""""
Na Mwandishi Wetu
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation wamesaini mkataba wa shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kuziwezesha biashara changa za vijana nchini. Hafla hiyo ya kihistoria imefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, ambapo rasmi ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Akihutubia katika hafla hiyo, Prof. Mkenda ameipongeza COSTECH kwa hatua hiyo muhimu na kueleza kuwa uwekezaji katika ubunifu wa vijana kwani msingi imara wa uchumi wa baadaye wa Tanzania.
“Hii ni hatua ya kupongezwa inayochochea ukuaji wa uchumi wa ubunifu. Ushirikiano huu ni jibu la changamoto ya ukosefu wa ufadhili kwa vijana wabunifu, na unaonesha dhamira ya kweli ya serikali katika kujenga uchumi shindani wa viwanda unaoongozwa na ubunifu,” amesema Prof. Mkenda.
Amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza mchango wa sekta ya ubunifu kwenye uchumi wa taifa, na kuhakikisha wabunifu wanapata mazingira bora ya kuendeleza kazi zao kwa tija, huku wabunifu hao wakiahidi kutumia mikopo hiyo ipasavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema kuwa taasisi hiyo itaendelea kuweka mazingira bora ya kuwasaidia vijana kwa kuanzisha na kukuza biashara zao, huku akieleza ushirikiano huo ni muendelezo wa safari iliyoanza mwaka 2023 kwa lengo la kuunga mkono ndoto za vijana wengi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Bi. Tully Mwambapa, alisema kuwa ushirikiano huu ni sehemu ya dhamira ya Benki ya CRDB katika kujenga uchumi jumuishi unaowajumuisha vijana na wanawake waliopo pembezoni.
“Tangu kuanzishwa kwa IMBEJU, tumelenga kuwafikia waliokuwa wakikosa fursa rasmi za kifedha. kupitia mkataba huu mpya, tunatarajia kuwafikia vijana zaidi ya 1,000 kwa kuwapa mitaji, mafunzo ya ujasiriamali, na elimu ya fedha,” amesema Bi. Mwambapa.
Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa, zaidi ya vijana 700 wabunifu wamewezeshwa kupitia dirisha la IMBEJU BUNI, ambapo mitaji ya thamani ya shilingi bilioni 5 imetolewa kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Kwa hatua hiyo, Tanzania inaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa ubunifu na ujasiriamali wa vijana, huku sekta ya fedha na teknolojia zikishirikiana kwa karibu katika kufanikisha ndoto za kizazi kijacho cha wajasiriamali.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Mwambapo (kushoto), wakionyesha mikataba baada ya kusaini makubaliano ya utoaji wa mikopo nafuu kwa wabunifu wa Tanzania, hafla hiyo imefanyika leo Aprili 17, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, akisisitiza jambo wakati wa hafla ya utiaji saini ya makubaliano ya utoaji wa mikopo nafuu kwa wabunifu wa Tanzania kati ya COSTECH na CRDB Foundation, hafla hiyo imefanyika leo Aprili 17, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akizungumza katika hafla ya utiaji saini ya makubaliano ya utoaji wa mikopo nafuu kwa wabunifu wa Tanzania kati ya COSTECH na CRDB Foundation.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, wakipokea mfano wa hundi ya shilingi bilioni 2.3 kutoka kwa Mkurugenzi wa Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Mwambapo kwa ajili ya kusaidia utoaji wa mikopo nafuu kwa wabunifu wa Tanzania.
Wafanyakazi wa COSTECH, CRDB Foundation, Tully Mwambapo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya utiaji saini ya makubaliao ya mikopo nafuu kwa wabunifu.
Baadhi ya picha za matukio mbalimbali katika hafla ya utiaji saini ya makubaliano ya utoaji wa mikopo nafuu kwa wabunifu wa Tanzania kati ya COSTECH na CRDB Foundation.
Post a Comment