MWENYEKITI WA CHADEMA MWANGA AOMBA MSAJILI KUTENGUA MAAMUZI YA BARAZA KUU, AKIDAI KASORO ZA KIKATIBA

*****

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Wilaya ya Mwanga Lembrus Mchome amesema amemuomba Msajili wa vyama vya siasa kutengua maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho yaliyofanyika kwenye kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika Januari 22, 2025 kwa kuwa kilikuwa na kasoro.

Akizungumza na wanahabari leo April 8, Mchome amesema Baraza kuu halikuwa halali kwani akidi haikutimia lakini pia ndani yake kulikuwemo na watu ambao sio wajumbe halali wa Baraza kuu kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA.

Mchome ameeleza kuwa amemuomba Msajili abatilishe vikao vyote vya kamati kuu viliyokaliwa kuanzia baada ya tarehe 22 kwani wajumbe wake akiwemo Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar uteuzi wao sio halali.

Aidha ameongeza kuwa amepokea barua leo kutoka kwa Msajili wa Vyama Vyama Siasa ikimjibu maombi yake kuwa Msajili amemtaka Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika kujibu malalamiko ya Mchome ndani ya siku tatu.

Katika hatua nyingine Mchome amesema anashangazwa na namna ambavyo Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu amekuwa akijibu wanachama wanaotoa maoni tofauti kuwa hatumii lugha nzuri wala namna nzuri.

Mchome amemtolea mfano Mwenyekiti aliyepita Freeman Mbowe kuwa alikuwa kiongozi ambaye alipokea maoni hata mbadala bila kuchukulia kwa ubaya “tulikuwa na Kiongozi aliyepita Mzee wetu Freeman Mbowe alikubali kupokea yote, alikubali kukosolewa aliyapokea yote”

 









 

0/Post a Comment/Comments