WAWEKEZAJI wa kigeni wameisifu Tanzania kwa kurahisisha mazingira ya uwekezaji hatua inayowawezesha kuanzisha na kusajili kampuni zao kwa haraka na kuanza shughuli rasmi bila vikwazo.
Akizungumza katika uzinduzi wa Tawi la Kampuni ya Teknlojia ya Spidd Africa nchini, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni hiyo, Catherine Kisaka, alisema Tanzania imeonesha nia ya dhati ya kuvutia wawekezaji kupitia sheria rafiki na mifumo rahisi ya usajili.
Kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Uganda, inalenga kukuza biashara na kubadilisha namna biashara zinavyoendeshwa kutumia suluhisho bunifu za kidijitali.
Kasanga amesema kuingia kwa kampuni hiyo nchini ni hatua muhimu kusaidia biashara barani Afrika kuongeza ufanisi, kuimarisha ulinzi wa kimtandao, na kustawi kidijitali kuanzia kwa wajasiriamali wadogo hadi kwa mashirika makubwa.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Spidd Uganda, Angela Semwogerere, alisema kuwa kampuni hiyo imejikita pia katika kutoa elimu na mafunzo kwa taasisi mbalimbali ili kukabiliana na changamoto za usalama wa kimtandao.
Semwogerere aliongeza kuwa Tanzania imekuwa kitovu muhimu cha maendeleo ya teknolojia na uchumi katika Afrika Mashariki, hali iliyochochea uamuzi wa kampuni hiyo kuwekeza nchini.
Post a Comment