WAKILI MWANAISHA MNDEME KUGOMBEA UBUNGE KIGAMBONI


                 :::::::

Wakili Mwanaisha Mndeme, Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje na Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara kupitia chama cha ACT-Wazalendo, amekabidhiwa rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni. Akizungumza na waandishi wa habari, Mwanaisha amesema anagombea kwa dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi wa Kigamboni na kuleta mageuzi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Ameainisha vipaumbele vyake ikiwemo kuboresha huduma za afya, elimu, miundombinu, na mazingira bora ya kiuchumi kwa vijana na wanawake. Pia amesisitiza kuifanyia kazi mikataba kandamizi inayowagharimu wananchi, mfano ada za matumizi ya Daraja la Mwalimu Nyerere, na changamoto za vivuko vinavyotegemewa na wakazi wa Kigamboni.

Mwanaisha amesema ubunge kwake si heshima ya kisiasa bali ni jukumu la utumishi wa kweli kwa wananchi. Amewataka wananchi kumpa nafasi ya kuwa sauti yao bungeni, akiwahakikishia kuwa atakuwa mtetezi wa haki na maendeleo jumuishi kwa wote.

Ametamatisha kwa kutoa wito wa umoja na mshikamano akisisitiza kuwa muda wa mabadiliko ni sasa, na Kigamboni inahitaji kiongozi kijana, makini na mwenye dira ya kweli ya maendeleo.









0/Post a Comment/Comments