ASKOFU NIWEMUGIZI ASISITIZA WAFANYAKAZI KULIPWA MISHAHARA MINONO

Mhashamu Askofu Severine Niwemugizi.

.................

Na Daniel Limbe,Chato

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, ameitaka serikali pamoja na waajiri viwandani kuwalipa mishahara minono wafanyakazi wao ili kuongeza ufanisi katika ajira.

Mbali na hilo ameiasa jamii kuondoa mtazamo hasi wa kuamini kazi bora ni za kuajiliwa kukaa ofsini pekee, badala yake wajikite kwenye kazi za mikono zinazoweza kuwapatia kipato cha kumudu maisha yao.

Amesema hayo leo wakati wakiongoza ibada maalumu ya siku ya wafanyakazi kwenye Kanisa la Bikira Maria wa Rozari Parokia ya Chato,ambapo amesisitiza kuwa kazi ni kipimo cha utu,heshima na maendeleo.

"Leo ni siku ya wafanyakazi, tunawakumbuka wafanyakazi kuwa wana haki mbalimbali zinazopaswa kutolewa kwao ikiwa ni pamoja na kuwaongeza mishahara na stahiki zingine ili kuwaongezea hali ya kupenda na kuthamini kazi wanazozifanya,"

"Hata Mungu alifanya kazi ya kumuumba mwanadamu,aliwaumba Adamu na Eva na baadaye kuwapa maagizo ya kufanya kazi na kuitiisha nchi,Yosefu alikuwa fundi seremara na alimfundisha Yesu kufanya kazi." amesema Niwemugizi.

Kwa mujibu wa Askofu Niwemugizi,kazi ni shughuli yoyote inayofanywa na mtu au kikundi chochote kinachowajibika kwa manufaa ya jamii, na kwamba hakuna sababu ya watu kubagua kazi.

"Upo mtazamo kwa baadhi ya watu kuwa kazi za ofsini ndizo zenye heshima kuliko za kawaida,huo ni mtazamo usio sahihi badala yake watu wanapaswa wafanye kazi hasa za mikono ili kujipatia kipato chao."

Aidha ameitaka serikali kuwapatia stahiki zao wafanyakazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, pamoja na wamiliki wa viwanda kuwapatia wafanyakazi wao mishahara inayotoshereza mahitaji ya kila siku.

Kadhalika amesisitiza wafanya biashara kujitakatifuza kwenye kazi zao kwa kufanya tathimini iwapo kazi hizo zina utukufu wa Mungu au ndizo zitakuwa chanzo cha kuwapeleka Jehanamu.

"Kazi yoyote unayoifanya ni muhimu Uipende na kuiheshimu,uifanye kwa Imani na maadili ili iweze kukufikisha katika utukufu wa Mungu.

Amehitimisha kwa kuitaka jamii kuacha kuwatumikisha watoto kazi ngumu za mitaani, badala yake wawafundishe kazi za nyumbani ambazo zimeruhusiwa na Sheria kulingana na umri wao na kuwapatia maadili mema.

           Mwisho.

 

0/Post a Comment/Comments