.....................
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, amekabidhi hundi zenye jumla ya Sh.bilioni 2.25 kwa wanufaika wa shughuli za utalii katika maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Wanufaika wa mgao huo ni pamoja na Jumuiya sita za Hifadhi za Wanyamapori (WMA) ambazo zimepokea Sh.bilioni 1.5, Halmashauri za Wilaya 20 ambazo zimepata jumla ya sh. milioni 368.7, na Halmashauri za Vijiji 25 ambazo zimepokea sh.milioni 385.5.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi hizo, Waziri Chana amesema kuwa ni ukweli usiopingika kwamba ongezeko la watalii nchini linaongeza mapato ya Serikali, ambapo sehemu ya mapato hayo yanarejeshwa kwa jamii kupitia migawo iliyoainishwa katika sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa utalii.
“Miongozo hiyo inaielekeza Serikali kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za utalii na kuyaelekeza kwa wanufaika – ambao ni halmashauri za wilaya, vijiji na WMA husika – kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii. Hafla hii ya kugawa mgao ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuzingatia sheria, uwazi na kuwajali wananchi wake,” amesema Waziri Chana.
Ameongeza kuwa fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo husika, na kutoa wito kwa vijiji, halmashauri, na hata Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kuweka ajenda ya utalii kwenye vikao vyao, ili kuhamasisha uanzishwaji wa WMA zaidi.
Aidha, Waziri Chana amesisitiza kuwa Wizara kupitia taasisi zake, hususan TAWA, itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha shughuli za utalii na kuhakikisha mgao unaowastahili wanufaika unatolewa kwa mujibu wa sheria.
Amesema serikali inatarajia kuona fedha hizo zinatumika kwa ufanisi na kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa – ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori, kukuza utalii na kuongeza mapato katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA.
Post a Comment