Na Daniel Limbe,Torch media
SERIKALI imezindua rasmi msimu wa ununuzi wa zao la pamba kwa mwaka 2025/26 huku ikitangaza bei elekezi ya shilingi 1,150 kwa kila kilogramu moja ya Pamba safi itakayouzwa na mkulima kwa wanunuzi binafsi na vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) kwa bei ya ushindani ili kuinua uchumi na tija kwa jamii.
Mbali na umuhimu mkubwa wa zao la pamba katika kukuza kipato cha familia, uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla, bado wapo baadhi ya wakulima ambao wamekuwa wakirudisha nyuma jitihada za serikali kwa kulichafua na kushusha ubora wake kutokana na imani potofu za kutumia mafuta ya kenge ili kuongeza uzito.
Kenge ni mnyama anayefanana na mamba mdogo kwa umbile, na hupenda kuishi nchi kavu pamoja na kwenye madimbwi ya maji, huku mafuta yake yakitajwa kuwa matibabu ya masikio.
Nikutokana na wataalamu wa tiba asilia kuamini kuwa mafuta ya kenge yanatibu ugonjwa wa sikio linalouma au kutokwa usaha.
Mbali na kuwa ni tiba ya ugonjwa wa sikio,baadhi ya wakulima wa zao la pamba wilayani ya Chato mkoa wa Geita, wanasema kuwa mafuta ya Kenge ni muhimu katika kuongeza uzito wa zao hilo na hivyo kuwaongezea kipato zaidi.
*Imani potofu*
Inaelezwa kuwa kuchanganya mafuta ya kenge kwenye zao la pamba ni imani potofu na ni kichocheo cha kuporomoka kwa bei na thamani yake ndani na nje ya nchi.
Uchunguzi umebaini uwepo wa mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya wakulima wa pamba kwa kuichanganya na mafuta ya kenge wakiamini kuwa huongeza uzito wakati wa kuuza zao hilo.
Baadhi ya wakulima wanaamini kuwa wakitumia mafuta ya kenge (Uru) kunyunyizia pamba safi iliyokwisha vunwa shambani kabla ya kufikishwa kwenye masoko ili kuuzwa huongeza uzito kwenye zao hilo kwa lengo la kujipatia fedha nyingi.
Mwandishi wa makala hii amefanikiwa kuzungumza na familia ya Nyangeta Masatu, ambaye ni mkulima wa pamba kwa zaidi ya miaka 37, bila shaka anakiri kuwepo kwa tabia hiyo kwa baadhi ya wakulima wa pamba.
Anasema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuamini kuwa mafuta hayo huongeza uzito wa pamba, hivyo kumsaidia mkulima kupata kilo nyingi anapouza pamba yake.
Anataja namna ambavyo mafuta hayo hutumika na kusema kuwa hupakwa kwenye pindo za shuka (nguo) inayotumika kuuzia pamba kabla ya zao hilo kupandishwa kwenye mzani wa kupimia uzito.
Masatu anasema kuwa njia nyingine ni kupaka mafuta ya kenge kwenye jiwe dogo ambalo huwekwa ndani ya kifungashio kilichobeba pamba hiyo.
Ernest Philipo, mkazi wa Nyarubungo anasema uharifu wa kutumia mafuta ya kenge aliushuhudia mwaka 1976 baada ya rafiki yake kutumia wakati wa msimu wa mauzo ya pamba.
Anasema pamoja na kuwa yeye hakuwahi kutumia mafuta hayo ila anatambua kuwa baadhi ya wakulima wa zao hilo hutumia mafuta hayo kujiongezea kipato hasa wakulima waliopo maeneo ya ukanda wa ziwa viktoria.
Zacharia Kapandekado, mkazi wa kijiji cha Katemwa Muganza, anakiri baadhi ya wakulima kutumia mafuta ya kenge pamoja na maji kuongeza uzito wa pamba.
Anasema vitendo hivyo hufanyika kwa kificho kwa kuwa wanatambua wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, huku akidai wanafanya uharifu huo kutokana na kuwa na pamba kidogo ikilinganishwa na wenye pamba nyingi.
*Mwenyekiti CCU aeleza thamani ya Pamba*
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika Chato (CCU) Abed Busumilo, anasema kuwa zao la pamba lina manufaa makubwa kwa jamii iwapo usimamizi wake utaimalishwa kuanzia ngazi ya familia, kitongoji, kijiji, kata, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
Anasema kuwa usimamizi huo unapaswa kuenenda sambamba na miongozo na maelekezo ya serikali katika kuhakikisha elimu zaidi inaongezwa kwa wakulima,kupitia taasisi zake pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
Busumilo anasema pamba ina faida rukuki iwapo itatunzwa na kuvunwa vizuri kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo hicho na kwamba inapovunwa na kuuzwa mkulima huanza kunufaika moja kwa moja kwa kujipatia fedha.
Mbali na mkulima, makampuni nayo huchakata na kutengeneza nyuzi (robota) ambazo huuzwa kwenye soko la dunia na nyingine hubaki nchini kama mali ghafi ya viwanda vya kutengeneza nguo.
Anadai kuwa mbegu ya pamba hukamuliwa mafuta ya kupikia ambayo hupendwa sana na wananchi wengi kutokana na ubora wake huku makapi ya mbegu hizo yakitengenezwa chakula cha mifugo (mashudu) pia hukamuliwa na kutengenezwa sabuni za kufulia na kuoshea vyombo.
Halikadhalika magugu ya zao la pamba nayo yakitumika kama kuni za kupikia chakula hasa maeneo ya vijijini, hivyo kusababisha zao hilo kupata umaarufu kiasi cha kupewa jina la dhahabu nyeupe.
*Kauli ya Mkaguzi Ubora wa Pamba*
Ofisa Mkaguzi Ubora wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba(TCB) wilayani Chato mkoani Geita, Samweli Mdidi, anathibitisha kuwepo kwa uharifu huo kwa baadhi ya wakulima wenye kuamini kufanikiwa kwa kutumia mafuta hayo.
Licha ya baadhi ya wakulima kuamini hivyo, anasema imani hiyo haina ukweli wowote zaidi ya kusababisha kuozesha pamba.
"Ni kweli kuna hayo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wetu wa pamba, tunaendelea kukagua na kutoa elimu kwa wakulima kuachana na imani hizo potofu, maana hakuna ukweli wowote wa kilo kuongezeka iwapo mkulima atatumia mafuta ya kenge badala yake ni kuozesha pamba,"anasema Mdidi.
Anasema kuwa madhara mengine yanayoweza kutokea kutokana na uchafuzi huo ni kushuka kwa bei ya pamba kutokana na wanunuzi kupata hasara ya kununua pamba isiyokuwa na ubora pamoja na kushuka thamani ya robota zetu kwenye soko la dunia.
Balozi wa pamba nchini,Agrey Mwanri,anasema kilimo chetu ni duni kisicho kuwa na faida,kwa sababu siyo cha kibiashara bali cha kujikimu,na kwamba inatokana na wakulima wengi kupanda pamba bila kuzingatia vipimo vinavyoshauriwa na wataalamu.
"Wakulima wengi wanapanda kwa mfumo wa tupa mbegu tukutane wakati wa palizi, wataalamu wetu wa TARI wekuja na vipimo vipya vya kupandia pamba kwa lengo la kuongeza idadi ya mimea kwa eneo,kwa vipimo vipya vya futi moja shimo hadi shimo na futi mbili mstari hadi mstari mkulima atakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji mara mbili,"amesema
"Vipimo vya zamani vilimpatia mkulima mimea 22,222 kwa hekari moja,wakati vipimo vipya vitaongeza hadi kufikia miche 44,444 hii ikiwa ni hatua ya kwanza katika uboreshaji wa zao hilo badala ya wakulima kuamini katika mafuta ya kenge na kuharibu ubora za zao," amesema Mwanri.
*Ofisa Wanyama Pori*
Kwa upande wake, Daktari mwandamizi kitengo cha wanyama pori nchini, Dk.Emmanel Macha, anasema kitaalamu hakuna uhusiano wowote kati ya mafuta ya kenge na suala la kuongezeka uzito ndani ya pamba.
"Kwanza itambulike kuwa ili kupata mafuta hayo lazima kenge auawe, mbali na kuwa ni imani potofu zisizo kuwa na ukweli wowote lakini kuna wasiwasi kubwa ya kuwaangamiza wanyama hao wasio na madhara yoyote kwa jamii"anasema Dk. Macha.
"Suala hilo halihitaji hata elimu kubwa, kama wanapakashia mafuta hayo kwenye jiwe halafu uzito umaongezeka kwenye pamba basi watambue kinachokuwa kimeongeza ni jiwe wala siyo mafuta hayo."anasema
Aidha anawataka wakulima kuachana na imani hizo badala yake walime pamba kwa kuzingatia majira ya msimu wa kilimo, kuzingatia kanuni bora pamoja na kusikiliza na kuzingatia kwa kina ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo hatua itakayosaidia kupata tija.
*Mkurugenzi TCB*
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga, anasema kuwa umaskini wa wakulima wa pamba hausababishwi na ukosefu wa nguvu kazi bali nikutokana na tija ndogo inayotokana na kutozingatia kanuni za kilimo bora licha ya takribani watu 600,000 kujihusisha na kilimo hicho.
"Wanatumia nguvu nyingi bila maarifa hivyo kuwafanya mara nyingi kulalamikia bei ndogo hali inayosababisha kuuza hata pamba chafu,
"Bila kutatua tatizo la tija ndogo, hata bei ikipanda maradufu, bado umaskini hautaondoka, uzalishaji wa kilo 300 kwa ekari ni mdogo sana,
"Wakulima wengi wa pamba wamekuwa wakishindwa kuwapa ushirikiano wakaguzi wanapobaini kuwepo kwa pamba chafu katika vituo vya kuuzia pamba kwa kuhofia kutouza pamba yao, pasipo kujua kuwa pamba chafu ndiyo chanzo kikuu kinachofanya bei ya pamba kuporomoka kwenye soko la dunia"anasema Mtunga.
Mtunga anawataka wakulima kutoa ushirikiano kwa wadau wa pamba na serikali ili kuwa na uzalishaji wenye tija lakini pia wakulima wajiunge kwenye ushirika ili kuleta mabadiliko chanya badala ya kuendelea kuwa walalamikaji.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye tovuti ya TCB, Zao la pamba hulimwa katika mikoa 17 ya Tanzania bara,na kwamba hutengenezwa nyuzi (robota) na kuuzwa kwenye soko la dunia, ambapo serikali hujipatia fedha za kigeni na kuchangia uchumi wa taifa.
Inaelezwa kuwa mkoa wa Singida, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita, Tabora na Kigoma inazalisha aslimia 90 ya pamba mbegu yote inayolimwa nchini.
Huku aslimia 10 ya pamba mbegu ikilimwa na mikoa ya Kagera,Dodoma, Katavi, Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga, Manyara na Pwani.
Miongoni mwa mikakati ya serikali ni kukuza uzalishaji wa pamba kutoka wastani wa tani 300,000 hadi kufikia tani 1,000,000.
Hatua hiyo inakuja huku baadhi ya mataifa mengi duniani ikiwemo nchi ya Misri ambayo huzalisha kilo 2,000 kwa ekari tofauti na Tanzania ambayo inazalisha kilo 300 kwa ekari moja.
Tovuti hiyo inaonyesha kuwa tangu uzalishaji wa pamba uanze hapa nchini mwanzoni mwa karne ya 20, uzalishaji wa juu kabisa ulifikiwa msimu wa 2005/2006 ambapo jumla ya tani 376,000 sawa na robota 700,000 zilizalishwa.
*Waziri wa Kilimo*
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, anasema ili kuinua kilimo cha pamba nchini,serikali,wakulima na wadau wengine wa tasnia ya pamba ni muhimu kushirikiana ili kuboresha mnyororo wa thamani katika zao hilo.
"Serikali imeendelea kuweka ruzuku kwenye sumu,mbegu na kutoa vifaa mbalimbali vitakavyo saidia uongezaji thamani ya zao hilo kuanzia shambani hadi sokoni,"
"Ni muhimu wakulima wetu kuzingatia matumizi ya mbegu bora, mbolea, na teknolojia za kisasa katika kilimo cha pamba ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo." anasema Bashe.
Kadhalika ameitaka Bodi ya Pamba kuhakikisha inasimamia vyema masoko ya pamba na kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na ya haki kwa mazao yao,huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima na wawekezaji katika sekta ya pamba ili kuhakikisha tasnia hiyo inakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na ustawi wa wakulima.
Bashe anawataka wakulima wa pamba kutokubali kuibiwa na wanunuzi, na kwamba bei watakayoikuta kwenye vituo vya kununulia pamba haitakiwi mkulima kukatwa hata senti kwa madai serikali imetoa ruzuku kwa zao hilo.
Anasema Chato ni moja kati ya wilaya zilizokuwa zinalima pamba kwa wingi lakini zao hilo liliporomoka kutokana na sababu mbalimbali hali iliyosababisha kiwanda cha kuchakata pamba cha Chato Co-operative Union (CCU)kufa.
*Soko la Dunia na bei ya Pamba*
Katibu wa Chama Cha wanunuzi wa Pamba nchini (TCA) Boaz Ogolla, anasema bei ya pamba kutokuwa rafiki kwa mkulima ni kutokana na uhitaji wa soko la kimataifa na mwenendo wake.
"Kuna vigezo ambavyo vinaangaliwa kama vile bei ya mbegu inauzwaje huko kwenye soko la dunia,hivyo niwasihi wakulima walime kwa kufuata kanuni za kilimo bora hali itakayosaidia kuondokana na changamoto ya bei hata kama itakuwa chini" anasema Ogolla. wakulima.
Hata hivyo amewahakikishia wakulima kuwa Pamba yote safi itakayovunwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2025/26 itanunuliwa yote kwa njia ya ushindani kwa kuzingatia mwenendo wa soko la kimataifa.
*Nini kifanyike*
Baadhi ya wadau wa zao hilo akiwemo Siwema Nongejiwa, anashauri jamii iendelee kuelimishwa kuzingatia kanuni bora 11 za kilimo cha pamba kupitia maofisa ugani vijijini,ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata pembejeo mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Maofisa ugani kwa kushirikiana na ofisa maendeleo ya jamii vijijini wasaidie kuelimisha wakulima kujiepusha na imani potofu za kutumia mafuta ya kenge kuongeza uzito wa pamba.
Bodi ya pamba waendelee kukagua ubora wa pamba kabla na baada ya kununuliwa, hatua itakayosaidia kusafirisha pamba nyuzi zenye ubora unaotakiwa kwenye soko la dunia.
Wananchi wahamasishwe kuendelea kulima pamba, kutokana na kuwa ni zao la biashara lenye manufaa rukuki kwa manufaa ya kaya na serikali.
Silvester John,anasema serikali iweke ruzuku kwenye zao la pamba ili kuwa na bei yenye tija kwa wakulima badala ya kutegemea msimamo wa kupanda au kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia, hali itakayo wavutia wakulima wengi kuendelea na kilimo hicho.
Mwisho.
Post a Comment