MADIWANI CHATO WALILIA SAFARI ZA NDEGE

:::::::

Na Daniel Limbe,Chato

BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita,limedai kusikitishwa na ukimya wa serikali kushindwa kurusha ndege kwenye uwanja wa ndege wa mkoa wa Geita uliopo Chato hali inayosababisha unyonge na usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Mbali na wananchi, safari za madaktari Bingwa na bobezi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufika kwenye hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) zimekuwa kero kwa wataalamu hao na kusababisha baadhi ya wagonjwa kutumia gharama kubwa kusubiri huduma za afya kutoka kwa wataalamu hao.

Kutokana na hali hiyo,madiwani hao wameiomba serikali kurudisha huduma ya usafiri wa ndege kwenye uwanja huo ili kupunguza kero na kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wa mkoa wa Geita na mikoa jirani.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Christian Manunga, amesema hayo kwenye kikao cha robo ya tatu ya Baraza la madiwani kilicholenga kupitia,kujadili na kushauri mambo mbalimbali ya maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Bwera, Josephat Manyenye,amesema kukosekana kwa usafiri wa ndege kwenye mkoa huo umesababisha hasara kubwa kwa baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakisafiri kwaajili ya kusafirisha na kuleta bidhaa mbalimbali kutoka China pamoja na Jijini Dar es salaam.

Amesema hatua hiyo pia imekuwa ni adha kubwa kwa baadhi ya wagonjwa waliokuwa wanalazimika kwenda Hospitali ya taifa ya Muhimbili kwaajili ya kuhudhuria matibabu yao.

Pamoja na mambo mengine, amesema serikali imewekeza kiasi cha zaidi ya Bilioni 49 katika ujenzi huo ili kurahisisha usafiri wa anga kwa wananchi waliopo pembezoni mwa nchi ikiwemo Chato,lakini ni ajabu kwa baadhi ya viongozi wa serikali kushindwa kurusha ndege eneo hilo licha ya kuwepo kwa abiria wa kutosha.

Halikadhalika wameiomba serikali kupeleka meli kwenye Bandari ya Nyamirembe ili kurahisisha usafiri kwa wananchi waliopo kwenye maeneo ya ukanda wa ziwa ikiwemo wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao kwenye visiwa.

Diwani wa kata ya Buseresere,Godfrey Miti,ameitaka serikali kuja na majibu ya kuridhisha sababu za kushindwa kurusha ndege kwenye uwanja huo,huku akidai kuwa wafanyabiashara wa Madini wa mkoa wa Geita wanahofia maisha yao kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika wa ndege ukilinganisha na awali wakati huduma hiyo ikitolewa eneo hilo.

"Tuombe serikali itupe majibu ya kwanini hawaleti ndege kwenye uwanja wetu wa mkoa wa Geita, maana awali tulikuwa kukifanya biashara na wenzetu wa Geita,Bukoba,Biharamulo na Ngara kusafirisha Madini yetu kupitia uwanja huo,na ilikuwa ukichelewa kidogo hupati tiketi, hiyo ni tafsiri kuwa abiria walikuwa wengi." amesema Miti.

Safari za ndege kwenye uwanja wa mkoa wa Geita,zimesimama kwa zaidi ya miezi sita huku jamii ikiwa haijui hatma ya usafiri huo kutokana na kutokuwepo kwa maelezo ya kina kutoka kwa Mamlaka husika.                         


Mwisho
 

0/Post a Comment/Comments