MKE WA RAIS WA MSUMBIJI AAHIDI USHIRIKIANO WA HUDUMA ZA AFYA NA JKCI

:::::::

Mke wa Rais wa Msumbiji, Bi. Gueta Selemane Chapo, ameonyesha nia ya dhati ya kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kuimarisha huduma za afya nchini mwake, hususan katika tiba ya moyo na upandikizaji wa mimba (IVF).

Akiwa katika ziara ya kutembelea JKCI na kueleza kuvutiwa kwake na uwezo mkubwa wa taasisi hiyo kuhudumia zaidi ya wagonjwa wa nje 2,000 na kulaza hadi wagonjwa 100 kwa wakati mmoja.

"Huduma zinazotolewa hapa ni za kiwango cha juu. Tunatamani kuona ushirikiano baina ya Hospitali ya Maputo na taasisi hizi ili nasi tuweze kuwahudumia akinamama na dada zetu katika maeneo yote ya nchi yetu – kusini, kati na kaskazini," alieleza Bi. Chapo.

Aidha, aligusia mafanikio ya huduma za upandikizaji mimba zinazotolewa Tanzania, akisema kuwa wamejifunza mengi kuhusu jinsi wanawake wasio na uwezo wa kupata watoto wanavyosaidiwa. Aliongeza kuwa wanatarajia kutuma ujumbe maalum kutoka Msumbiji ili kuja kujifunza zaidi nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alisema Bi. Chapo amepata fursa ya kujionea teknolojia ya kisasa inayotumika kuwafuatilia wagonjwa waliopata upasuaji, hata wakiwa majumbani mwao kupitia mashuka maalum yenye uwezo wa kupima taarifa muhimu za kiafya.


 







0/Post a Comment/Comments