NIDA YAKAMATA MTUHUMIWA WA KUTENGEZA VITAMBULISHO FEKI VYA TAIFA

:::::;

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kumtia mbaroni mtu mmoja anayesadikiwa kujihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vitambulisho feki vya Taifa kwa malipo ya kati ya shilingi 6,000 hadi 10,000.

Akizungumza na waandishi wahabari Leo Jijini Dar es Salaam Msemaji Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano NIDA Geofrey Tengeneza amesema mtuhumiwa, Danford Mathius, mkazi wa Chanika, Ilala, alikamatwa Aprili 23, 2025 katika studio yake ya Bwanga iliyopo Msata, Chalinze.

Inadaiwa alikuwa akitumia kitambulisho chake halali cha NIDA kuingiza taarifa kwenye mfumo wa RDDB na baadaye kuweka taarifa za uongo za wateja wake kama vile majina, picha, NIN, saini, na tarehe ya mwisho wa matumizi.

NIDA imesema operesheni ya kuwakamata watu wanaojihusisha na uhalifu huu ni endelevu nchi nzima na imeahidi kuwa hakuna atakayesalimika mkono wa sheria.

Aidha, mamlaka hiyo imewaonya wamiliki wa maduka ya vifaa vya elektroniki kujiepusha na utengenezaji au uchapishaji wa vitambulisho bandia, ikisisitiza kuwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na hayo amewataka Wananchi  kutotumia njia zisizo rasmi kupata huduma za NIDA, kwani kitambulisho cha Taifa kinachotolewa kwa mara ya kwanza ni bure.

Hata hivyo NIDA imeeleza kuwa ujumbe mfupi (sms) wa kuwajulisha wananchi kuchukua vitambulisho vyao ni halali na kuwa kufungwa kwa namba ya usajili haina maana kuwa kitambulisho hakitatolewa – bali namba hiyo itahuishwa mwananchi atakapojitokeza kukichukua.

0/Post a Comment/Comments