SERIKALI YAMPONGEZA MWL BHOKE KINARA UPISHI NA UPAMBAJI GEITA

...................

Na Daniel Limbe,Torch media

SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imempongeza Bhoke Kisigiro, kwa kuibuka mshindi wa kwanza katika tuzo ya mpishi na mpambaji bora wa keki 2025 iliyotolewa na "Geita Women Festival (GWF) huku watumishi wengine wakihimizwa kufanya shughuli za ziada za kuwaingizia kipato baada ya muda wa kazi.

Bhoke ambaye kitaaluma ni mwalimu, amefanikiwa kutwaa tuzo hiyo baada ya kupigiwa kura nyingi kuliko washindani wake hali iliyomfanya kuibuka kinara wa kipengele hicho.

Akitoa pongezi za serikali, mkuu wa wilaya ya Chato Louis Peter Bura, amesema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa wananchi wa wilaya ya Chato na mkoa mzima wa Geita na kwamba inapaswa kuwa chachu kwa watu wengine katika kuthubutu na kuboresha kazi zao za kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa mtumishi wa Umma isiwe kikwazo cha kujitafutia maendeleo nje ya utumishi ispokuwa baada ya kazi za mwajiri ni vizuri kuwa na kazi ya ziada inayoweza kukuongezea kipato halali ili kujikwamua kimaendeleo.

Hata hivyo amemtaka mshindi huyo kuendeleza mahusiano mema kwa watumishi wenzake na jamii inayomzinguka ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii ndani na nje ya kazi za utumishi wa umma.

Akipokea pongezi za serikali, Bhoke amewashukuru watanzania wote waliompigia kura wakiwemo wananchi wa wilaya ya Chato ambao kwa moyo wa dhati waliguswa na kazi nzuri anazofanya katika jamii huku akiahidi kuboresha zaidi ili jamii iendelee kunufaika na kazi zake.

Kadhalika ameishukuru Ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kwa uhusiano mwema na jamii, hatua iliyosaidia yeye kufika katika Ofisi hiyo kwa lengo la kuitambulisha tuzo hiyo ambayo inafungua milango kwa wajasiliamali wengine kuboresha kazi wanazozifanya kwa manufaa ya jamii.

Baadhi ya wadau wa mapambo akiwemo Leah Mgogo ,amedai kuguswa na mafanikio ya Bhoke baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika kinyang'anyilo hicho na kwamba jamii haina budi kuendelea kumuunga mkono katika kazi zake..

                        Mwisho.

0/Post a Comment/Comments