:::::::::
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) umezindua basi lake la kwanza linalotumia gesi asilia iliyosindikwa (CNG), hatua inayolenga kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha mazingira ya usafiri jijini Dar es Salaam,Uzinduzi huo umefanyika katika kituo cha TPDC, ukiashiria mwanzo wa mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa umma,basi hilo ni la kwanza kati ya mabasi 100 yanayotarajiwa kuwasili nchini kabla ya Agosti mwaka huu.
Mkurugenzi wa UDART, Bw. Waziri Kindamba, amesema basi hilo limeletwa kwa ajili ya majaribio na litaanza kutoa huduma kuanzia Jumatatu, likisafirisha abiria kutoka Morocco hadi Kivukoni bila malipo kwa wiki moja kwa wale wenye kadi za UDART. “Ni mwanzo wa mabadiliko ya kweli katika mfumo wetu wa usafiri. Lengo ni kuhakikisha abiria wanapata huduma bora na ya kisasa,” alisema.
Basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 155 lina vifaa vya kisasa vikiwemo kiyoyozi na sehemu za kuchajia simu, jambo ambalo linalenga kuongeza faraja kwa wasafiri. Bw. Kindamba alisisitiza kuwa joto la Dar es Salaam halitakuwa tena kero kwa abiria na kwamba huduma hiyo itawavutia wengi kutumia usafiri wa umma.
Ingawa mabasi ya gesi hayawezi kutatua changamoto zote za usafiri jijini, yanatazamwa kama hatua muhimu katika kupunguza msongamano na adha kwa wasafiri. UDART ina mpango wa kuyabadilisha mabasi ya zamani kwa awamu huku ikiendelea kushirikiana na waendeshaji binafsi. Utafiti wa mwaka 2017/18 ulionyesha mahitaji ya zaidi ya mabasi 260 kwa ufanisi, lakini hadi sasa ni chini ya 100 yanayotoa huduma.
Post a Comment