AIRTEL, NEMC WAFANYA USAFI MBEZI BEACH, WAAHIDI KUDUMISHA UHIFADHI WA MAZINGIRA



Na Mwandishi Wetu, 

Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na wadau wengine wa mazingira, jana Juni 13, 2025 waliendesha zoezi la usafi katika fukwe za Mbezi Beach B, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kutunza mazingira ya baharini.

Zoezi hilo lililowashirikisha wakazi wa eneo hilo, wafanyakazi wa Airtel pamoja na maofisa wa NEMC, lililenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira hasa katika maeneo ya fukwe yanayokumbwa na utupaji wa taka kiholela.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Udhibiti wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano alisema kuwa kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhifadhi mazingira kwa kutoa elimu kwa njia ya ujumbe mfupi kwa wateja wake, hasa katika mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa taka.

“Tunaamini kwamba mazingira safi ni msingi wa afya bora na ustawi wa jamii. Airtel itaendelea kuwekeza katika miradi ya kijamii inayolenga kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Beatrice.

Katika hatua ya kuunga mkono juhudi hizo, Beatrice aliongoza wafanyakazi wa Airtel kugawa vifaa vya kuhifadhia taka kwa wakazi wa Mbezi Beach B, na kuwaasa kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi wa mara kwa mara si tu kwa ajili ya viumbe wa baharini bali pia kwa afya zao binafsi.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Beatrice alibainisha kuwa mazungumzo rasmi na NEMC yanapangwa kufanyika ili kubuni mkakati wa kufanya kampeni hiyo kuwa endelevu na yenye matokeo ya muda mrefu kwa mazingira.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa NEMC Kanda ya Mashariki, Jeremiah Nyakwaka, alizitaka taasisi na viwanda vinavyozalisha taka hatarishi kama plastiki na makopo kuhakikisha vinazihifadhi kwa njia salama ili kuepuka madhara kwa mazingira ya bahari.

“Taasisi binafsi na wananchi kwa ujumla tunapaswa kuwa mabalozi wa mazingira. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunalinda rasilimali hizi muhimu kwa maisha ya sasa na ya baadae,” alisema Nyakwaka.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Beach-B, Asha Vionatis, aliipongeza Airtel na NEMC kwa ushirikiano wao, akisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa afya ya jamii na maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta ya uvuvi.

“Takataka zinazoingia baharini huathiri moja kwa moja viumbe kama samaki, ambao ni chanzo kikuu cha kipato kwa jamii yetu. Zoezi hili linapaswa kuwa endelevu,” alisema Vionatis.

Zoezi hilo limepokelewa kwa matumaini makubwa na wakazi wa Mbezi Beach B, wakieleza kuwa linaongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za uharibifu wa mazingira na kuhamasisha tabia chanya ya utunzaji wa fukwe.





























0/Post a Comment/Comments