Na Mwandishi Wetu,
Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania,
kupitia huduma yake ya Airtel Money, imetangaza uzinduzi rasmi wa huduma ya
kadi ya malipo ya kimataifa kwa njia ya kidijitali, ijulikanayo sasa kama Airtel
Money Global Pay.
Huduma hiyo mpya imezinduliwa kwa
ushirikiano kati ya Airtel Money, Mastercard na kampuni ya teknolojia ya malipo
ya kimataifa ya Network International. Kupitia huduma hiyo, wateja wa Airtel
sasa wataweza kufanya malipo ya kimataifa moja kwa moja kutoka kwenye simu zao
za mkononi, bila kuwa na akaunti ya benki.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi
iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa
Bodi ya Airtel Money, Adolf Kasegenya, alisema huduma hiyo inaendana na juhudi
za Serikali kuhimiza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali.
“Huduma hii ni sehemu ya kuunga mkono
ajenda ya kitaifa ya kukuza uchumi wa kidijitali, ambapo sasa Watanzania
wanaweza kufanya manunuzi, kulipia masomo, au huduma nyingine popote duniani
kwa usalama na urahisi,” alisema Kasegenya.
Airtel Money Global Pay inapatikana kupitia
programu ya MyAirtel App, na inamwezesha mtumiaji kujipatia kadi ya kidijitali
papo hapo, kuijaza salio kupitia Airtel Money, na kufanya miamala ya kimataifa
kwa kutumia sarafu mbalimbali huku viwango vya ubadilishaji wa fedha vikiwa
vinaonekana moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Airtel Money
Tanzania, Bw. Andrew Rugamba, huduma hiyo imeboreshwa zaidi ili kutoa suluhisho
la uhakika kwa Watanzania wanaofanya manunuzi na shughuli mbalimbali mtandaoni.
“Watumiaji hawahitaji tena akaunti ya
benki. Unachohitaji ni kupakua MyAirtel App, kuomba kadi yako ya Global Pay,
kuweka salio, na kuanza kutumia huduma hii kulipia bidhaa na huduma kutoka kote
duniani,” alisema Rugamba.
Ameongeza kuwa huduma hiyo ni mkombozi kwa
Watanzania ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbana na changamoto za kufanya
malipo ya kimataifa, ikiwemo kadi kutokubalika, ukosefu wa uwazi kwenye viwango
vya kubadilisha fedha, na hofu ya usalama wa taarifa za kifedha.
Kwa mujibu wa Airtel, huduma hiyo pia
inamwezesha mtumiaji kudhibiti matumizi kwa wakati halisi, kusitisha miamala
kwa urahisi, na hata kubadilisha mwonekano wa kadi kupitia simu yake.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa
Mastercard kwa Ukanda wa Telco EEMEA, Kirsten Wottman*, alisema ushirikiano wao
na Airtel unalenga kuhakikisha huduma za kifedha salama zinawafikia watu wengi
zaidi katika masoko yanayoendelea kama Tanzania.
“Tunataka kuhakikisha kila Mtanzania
anapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia kupitia miamala
salama, hata kama hana akaunti ya benki,” alisema Wottman.
Uzinduzi wa Airtel Money Global Pay pia umekuja na mabadiliko ya jina kutoka "Airtel Mastercard" hadi jina jipya, huku maboresho zaidi yakijumuisha usalama wa miamala, utumiaji rahisi, na urahisi wa kuunganishwa na huduma nyingine za Airtel Money.
Huduma hiyo mpya inatarajiwa kusaidia makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wafanyabiashara wa mtandaoni, watumiaji wa huduma za burudani, na wasafiri wanaohitaji kufanya malipo ya haraka, salama na kwa gharama nafuu.
Post a Comment