Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema miongoni mwa maboresho yaliyofanyika katika mitaala ya mwaka 2023 ni pamoja na kuchopeka matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.
Dkt. Komba ameeleza hayo Juni 14, 2025 jijini Dar es Salaam akizungumza katika Hafla ya Utoaji wa Zawadi kwa Washindi wa Shindano la Tatu la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Elimu ya Msingi na la Kwanza kwa Walimu wa Sekondari, ambapo amesema kuwa shindano hilo ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa.
‘’Shindano hili linalenga kutoa fursa kwa walimu wa somo la Sayansi kwa elimu ya msingi na masomo ya Sayansi na Hisabati kidato cha kwanza kuonesha umahiri wa kutumia TEHAMA na mbinu shirikishi katika ufundishaji ili kukuza stadi za karne ya ishirini na moja" alisema Dkt. Komba.
Mkurugenzi huyo ameishukuru Benki ya Dunia, kwa kutambua umuhimu wa shindano hilo na kuendelea kulifadhili kupitia Miradi ya BOOST na SEQUIP, inayolenga kuimarisha uwezo wa walimu katika ufundishaji na ujifunzaji kupitia Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA).
Walimu kumi wa shule za msingi na sekondari wameibuka washindi katika Shindano la Stadi za Ufundishaji kwa masomo ya Kemia, Fizikia, Baiolojia na Hisabati.
Mshindi wa kwanza kwa kila somo amepata Sh. milioni nne (4,000,000), mshindi wa pili milioni tatu (3,000,000), mshindi wa tatu milioni mbili na nusu (2,500,000), wa nne milioni mbili (2,000,000), huku mshindi wa tano hadi wa kumi Sh. milioni moja (1,000,000) kila mmoja.
Post a Comment