Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Kukamilika kwa Kituo cha Biashara na Uwekezaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam, kunatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara kati ya mataifa ya Afrika Mashariki, kufuatia uwezo wake wa kuhudumia zaidi ya wafanyabiashara 2,000 ndani ya jengo hilo la kisasa.
Kituo hicho kinatajwa kuwa moja ya maeneo muhimu ya kimkakati kwa biashara za kikanda, kikilenga kuwaunganisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kiteknolojia.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano kati ya kituo hicho na kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa Yas, Pierre Canton Bacarapa, na Mkurugenzi wa huduma ya malipo ya kidijitali Mixxy by Yas, Angelika Pesha, walisema ushirikiano huo utaimarisha huduma za mawasiliano na miamala kwa njia ya kidijitali ndani ya kituo hicho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa EACLC, Cathy Wang, alisema kituo hicho sasa kinajipanga kuanza kutumia teknolojia ya akili bandia (AI) katika kutoa huduma kwa wafanyabiashara, ili kwenda sambamba na mahitaji ya kisasa ya kiteknolojia na kuongeza ufanisi wa huduma.
Alisema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya EACLC kuwa jukwaa la kisasa na jumuishi kwa ajili ya kukuza biashara, ubunifu na uchumi wa kikanda.
Kituo hicho kinatarajiwa kuwa kichocheo cha ajira, ubunifu wa biashara, na maendeleo ya kiuchumi kwa Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Post a Comment