MKAKATI WA TAIFA WA MAWASILIANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA WAZINDULIWA

:::::::

Na Ester Maile Dodoma 


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia, pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na hivyo kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kuhamia katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.

 Amezidua Mkakati huo wa Mawasiliano jijini Dodoma, tarehe 2 Juni 2025, Dkt. Biteko ameagiza kuwa mkakati huo usiishie kukaa kwenye makabati bali utekelezwe katika ngazi zote za Serikali hadi ngazi ya mtaa bila kusahau Sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya Habari kuwa mstari wa mbele katika kuutekeleza.

Katika uzinduzi huo, Dkt. Biteko amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara namba moja wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi ambapo kutoka azindue Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024-2034) mnamo tarehe 08 Mei, 2024 matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6 hadi 16. 



Dkt. Biteko ameeleza kuwa, matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia yanaendelea kuathiri afya na maisha ya watumiaji wengi hasa kina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambapo taarifa zinaonesha kuwa, watu bilioni 2.1 sawa na asilimia 24.7 ya Watu wote Duniani hawana nishati safi ya kupikia ambapo kati yao watu Milioni 990 sawa asilimia 47.1 ya wanaotumia nishati isiyo salama wanatoka barani Afrika. 

 Afrika inalazimika kufunga mkanda katika safari ndefu ya kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambapo kwa upande wa Tanzania kila Taasisi inapaswa kutambua na kutekeleza jukumu lake kikamilifu.

Dkt. Biteko amewasisitiza Wadau wote wanaohusika na Nishati Safi ya Kupikia kuhakikisha kuwa wanandaa na kutekeleza Kampeni zinazolenga makundi maalum katika jamii, kukuza uelewa wa umma kuhusu njia za ufadhili na gharama nafuu, kuhakikisha ujumbe thabiti wenye kueleweka unafika kwa wadau wote na kuendeleza na kuimarisha njia za mawasiliano za kuaminika. 

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji kufanya tathmini katika kila robo mwaka ili kuweza kujipima juu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.::::::




0/Post a Comment/Comments