Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Dar es Salaam imekuwa mwenyeji wa mkutano muhimu wa kimataifa wa kujadili maboresho ya mikataba ya nyuklia, kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nyuklia kwa usalama pamoja na kuhakikisha matumizi yake yana manufaa ya kijamii na kiuchumi. Mkutano huo umezikutanisha nchi 15 kutoka Ukanda wa Afrika.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, alisema mkutano huo umeandaliwa kwa kushirikiana na Wakala wa Nguvu za Nyuklia Duniani (IAEA) kwa lengo la kulinda vyanzo vya nyuklia na kuhakikisha matumizi yake hayaleti madhara kwa binadamu na mazingira.
“Leo tumekutana kwa ajili ya maboresho ya mkataba wa nyuklia ili kila nchi iweze kutekeleza miradi yake kwa kuzingatia usalama. Huu ni mkutano wa kimataifa unaolenga hatua ya kwanza ya kuhakikisha vyanzo vya nyuklia vinatumika kwa manufaa pasipo madhara,” alisema Prof. Mushi.
Aidha, Prof. Mushi alibainisha kuwa yapo masharti muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na nchi zote wanachama, akisisitiza kuwa teknolojia hiyo ya nyuklia ni lazima iwanufaishe wananchi na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania (TAEC), Profesa Najat Kassim Mohamed, alisema kuwa mikakati mbalimbali ya kimataifa imeandaliwa ili kuhakikisha matumizi salama ya nguvu za nyuklia, ambapo utekelezaji wake unaweza kuchukua kati ya miaka saba hadi kumi.
“Tanzania ina vyanzo mbalimbali vya nyuklia ambavyo vinaweza kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi. Kupitia mkutano huu, tunaweka mikakati ya pamoja na kuhamasisha nchi wanachama kusaini mikataba husika,” alieleza Profesa Najat.
Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ya kimkakati kwa mataifa mengine yasiyo na bandari, hivyo hutumika kama njia muhimu ya kupitisha vifaa na malighafi za nyuklia kwa kufuata taratibu za kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, John Simba Chaka, alisema kuwa mkutano huo ni fursa ya kipekee ya kubadilishana uzoefu kuhusu taratibu za usafirishaji wa madini ya nyuklia ambayo hutumika katika sekta mbalimbali duniani.
Mkutano huu unaonesha dhamira ya pamoja ya nchi za Afrika kulinda, kusimamia, na kutumia rasilimali za nyuklia kwa usahihi ili kuchochea maendeleo ya kisayansi, kijamii na kiuchumi kwa bara zima.
Post a Comment