:::::::::
Imeelezwa kuwa licha ya maendeleo makubwa katika sayansi na teknolojia ya nyuklia, ushiriki wa wanawake bado ni mdogo kutokana na changamoto mbalimbali, zikiwemo idadi ndogo ya wasichana wanaochagua masomo ya sayansi, mitazamo ya kijamii, na ukosefu wa mifano ya kuigwa.
Hayo yameelezwa Juni 4, 2025 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, wakati akizindua Jumuiya ya Wanawake katika Nyuklia Tanzania (WiNTz) ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta hii muhimu.
Prof. Nombo amesema kuwa tatizo hilo ni changamoto ya kimataifa, lakini athari zake ni kubwa zaidi katika nchi zinazoendelea.
Ameongeza kuwa WiNTz kimeanzishwa ili kusaidia juhudi za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) katika kuwawezesha wanawake kwenye sekta ya nyuklia na kuhimiza usawa wa kijinsia katika sayansi na teknolojia. Kwa mujibu wa Prof. Nombo, Jumuiya hii itasimamiwa na Tume ya Nishati ya Atomiki ya Tanzania (TAEC) chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Ameeleza kuwa WiNTz siyo tu Jumuiya, bali ni jukwaa la uwezeshaji, ujumuishi, na ubora ambalo litawezesha wanawake kushiriki maarifa, kusaidiana, na kuleta mabadiliko chanya. Kupitia mpango wa uelekezaji, utetezi, na ushirikiano, chama kitalenga kuwapa wanawake fursa za kitaaluma katika sekta ya nyuklia, ikiwa ni hatua muhimu katika kuinua ushiriki wao na kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kitaaluma.
Kiongozi huyo amesisitiza kuwa hatua hii inaleta matumaini mapya kwa maendeleo ya teknolojia ya nyuklia nchini na nafasi zaidi kwa wanawake katika nyanja hii yenye umuhimu mkubwa.
PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY
Post a Comment