::::::::::
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Shirika la Viwango Tanzania kutokuwa na huruma na bidhaa zisizokuwa na ubora kwani Serikali inataka soko la Tanzania liwe na bidhaa bora, salama na zenye kuleta tija kwa mlaji na kwa uchumi.
Amewataka wazalishaji wa bidhaa na huduma, wahakikishe wanazingatia taratibu za vipimo, uthibitishaji wa ubora, na uboreshaji wa mifumo ya uzalishaji. “Muhakikishe bidhaa zenu zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa vilivyowekwa na TBS”.Ametoa maagizo hayo, Juni 4, 2025) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jingo la maabara na ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kufuatwa kwa viwango vya ubora.
Waziri Mkuu pia ametoa wito kwa wafanyabiashara na waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, wakuwa na wajibu wa kuhakikisha bidhaa wanazoingiza nchini ni salama, zimeidhinishwa na zina alama ya ubora kutoka TBS au taasisi zinazotambulika.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua kuwa viwango vya ubora si tu vinahusiana na bidhaa bora, bali vinaimarisha afya na uchumi imara wa nchi. “Viwanda vyetu vinapaswa kuzalisha bidhaa ambazo zinaweza kununulika hata nje ya nchi, tunataka mataifa mengine yakimbilie bidhaa zetu.”
Amesema mradi huo unakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya afya kupitia usimamizi wa ubora wa bidhaa, vifaa tiba, vyakula, vipodozi na kemikali mbalimbali. “TBS ni mlinzi wa viwango; na kwa miundombinu hii mipya, huduma zitaimarika na kuchangia kulinda afya za wananchi.”
Post a Comment