::::::::
Na Mwandishi wetu Dar es dsalaam
Wajasiriamali wapatao 400 kutoka sehemu mbalimbali nchini wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wajasiriamali wa Biashara Ndogo na za Kati, yatakayofanyika Juni 27, mwaka huu, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), yakiwa na lengo la kuongeza mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi jumuishi na maendeleo ya taifa.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, likiwemo Benki ya Maendeleo ya TIB, na yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la majadiliano, mafunzo na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wajasiriamali wa viwango tofauti.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja wa SIDO Mkoa wa Dar es Salaam, Hopeness Elia, alisema lengo kuu la tukio hilo ni kutambua na kusherehekea mchango mkubwa wa wajasiriamali wadogo na wa kati katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo endelevu nchini.
“Wajasiriamali hawa si watu wa pembeni tena, bali ni injini ya uchumi. Tunaamini kupitia maadhimisho haya, tutatoa dira mpya kwao ili waendelee kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Elia.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mawasiliano kwa Umma na Masoko wa Benki ya Maendeleo ya TIB, Edward Kaguo, alisema benki hiyo imekuwa ikiunga mkono sekta ya ujasiriamali kwa kutoa elimu ya fedha, kuwajengea uwezo wa kunufaika na mikopo, pamoja na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kifedha na kibiashara.
“TIB imejikita katika kukuza maendeleo kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali, wajasiriamali wakiwa sehemu ya msingi ya mpango huo.
Tunaamini elimu na mitaji inayotolewa itawasaidia kufanikisha malengo yao ya kibiashara na kiuchumi,” alisema Kaguo.
Maadhimisho hayo yanakuja wakati ambao serikali na sekta binafsi zimeongeza juhudi za kukuza biashara ndogo na za kati kama njia mojawapo ya kutatua changamoto ya ajira na kuinua pato la taifa kupitia ubunifu wa ndani na viwanda vidogo.
PICHA ZOTE NA JAMES SLVATORY TORCHMEDIA
Post a Comment