Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa,amesema Serikali imedhamiria kujenga miundombinu ya mchezo wa Gofu.
Msigwa aliyasema hayo Septemba 20,2025 wakati akifunga mashindano ya Afrika Mashariki ya KCB Lugalo Golf Tour.
Aidha Msigwa aliipongeza menejment na wafanyakazi wa Benki ya KCB kwa kuwa na jicho kali kwa kuona fursa zilizopo katika sekta ya michezo na kuamua kufadhili na Kuendesha maonesho haya ambayo yanachagiza juhudi za uwekezaji mkubwa unaofanywa na mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan .
“Tukio hili linaonesha ushirikiano thabiti baina ya taasisi binafsi na serikali katika kuendeleza sekta Zinazorudisha manufaa na shukrani kwa jamii ikiwemo sekta ya michezo ambapo leo tunashuhudia kuhitimishwa kwa mashindano haya kwa udhamini wa Benki ya KCB “
“Tunakwenda kuongeza jitihada za kwenda kuongeza miundombinu ya mchezo huu, Dodoma, Songea, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza , Kigoma , morogoro na Mbeya “ Alisema Msigwa
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano na mahusiano Bank ya KCB, christina Manyeye alisema kuwa mashindano ya golf yaliyofanyika leo ni mwendelezo wa ahadi iliyotolewa mwaka jana kwamba yatakuwa endelevu.
Alieleza kuwa mbali na golf, pia wanadhamini michezo mingine ikiwemo Ligi Kuu ya England (Premier League).
Aidha, alieleza mashindano ya magari yanayofanyika mkoani Morogoro ambapo dereva wao, Karan Patel, ndiye bingwa wa Africa Rally Championship.
Kwa upande mwingine , alisema wamekuwa wakiangalia maendeleo ya watoto wadogo kupitia programu ya Young Golfers ambapo walitoa zawadi kwa washindi na wanapanga kuendesha clinic pamoja na kutoa elimu ya masuala ya kifedha kwa watoto hao ili wakue wakiwa wanariadha bora na wenye uelewa wa fedha.
Kadhalika alisema kuwa Tarehe 15 mwezi huu waliendesha kampeni ya kupanda miti 6,000 mkoani Mara kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, na wameahidi kuendelea na juhudi hizo za mazingira.
Mwenyekiti wa Lugalo Golf Club , Meja Jenerali Balozi Wilbert Ibunge alishukuru KCB Bank kwa kuendelea kuwa sehemu ya safari ya kuimarisha mchezo wa golf nchini Tanzania, akibainisha kuwa klabu hiyo si tu sehemu ya mazoezi kwa rika zote bali pia chachu ya kukuza vijana na wanawake ili waweze kufikia viwango vya juu vya kitaaluma katika mchezo huo.
Alitoa wito kwa wazazi kupeleka watoto wao kwenye klabu hiyo ili kujifunza mchezo wa golf kuanzia wakiwa wadogo.
Alisema ni fursa muhimu ya kuhakikisha watoto wanapata ujuzi na msingi mzuri wa mchezo huo.

Post a Comment