WATANZANIA WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZA MAENDELEO KUINUA UCHUMI – KAFULILA


::::::::::

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, amewataka Watanzania kuchangamkia kikamilifu fursa mbalimbali za kimaendeleo zilizopo nchini ili kuongeza kipato chao na kuchochea ustawi wa uchumi wa taifa kwa ujumla.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa kiuchumi ulioandaliwa na PPPC na kuhudhuriwa na wachambuzi wa masuala ya uchumi kutoka taasisi mbalimbali, Kafulila alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki zilizojaaliwa kuwa na rasilimali nyingi na muhimu, ambazo zikitumika kwa tija zina uwezo wa kubadilisha maisha ya wananchi na kuinua pato la taifa.

“Tuna ardhi ya kutosha, madini, gesi, na vivutio vya utalii. Fursa hizi ni msingi imara wa maendeleo endapo zitatumika ipasavyo. Tunahitaji kuwa na mtazamo wa pamoja katika kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na utajiri huu wa taifa,” alisema Kafulila.

Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma ni jambo la msingi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, huku akieleza kuwa ushirikiano huo ni kichocheo muhimu cha maendeleo na ajira kwa vijana.

“Sekta binafsi ni injini ya uchumi. Kwa kushirikiana na serikali, tunaweza kufanikisha miradi mikubwa kwa haraka zaidi, huku tukiwawezesha vijana kupata ajira na stadi za kazi,” aliongeza Kafulila.

Kwa upande wao, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi walioshiriki mdahalo huo walieleza kuwa mafunzo waliyopata yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, hususan katika kupanga sera na kutoa ushauri wa kitaalamu kwenye taasisi wanazozihudumia.

Mdahalo huo ni sehemu ya jitihada za PPPC za kuhamasisha ushirikiano baina ya sekta binafsi na ya umma katika kuchangia maendeleo ya taifa.


 

0/Post a Comment/Comments