BENKI YA KILIMO YASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA CHAKULA BORA KWA MAISHA YA BAADAYE


::::::::::::

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuchochea mapinduzi ya kilimo chenye tija nchini, wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Maadhimisho ya Chakula Duniani Kitaifa, yaliyofanyika leo katika viwanja vya Usagara jijini Tanga.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Buriani, aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujifunza na kushiriki mijadala ya kitaifa kuhusu usalama wa chakula na lishe bora, akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa katika kufanikisha ajenda ya chakula bora kwa wote.

Maadhimisho hayo ambayo yameanza jana, Oktoba 11, 2025, yanatarajiwa kuendelea hadi Oktoba 16, 2025, yakihusisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya chakula ndani na nje ya nchi. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tuungane Pamoja Kupata Chakula Bora kwa Maisha ya Baadaye,” ikilenga kuhimiza mshikamano, ubunifu, na uwajibikaji wa pamoja katika kujenga mifumo endelevu ya usalama wa chakula.

Kwa upande wake, TADB imesisitiza kuwa itaendelea kuwa chombo muhimu katika kufanikisha azma ya taifa kujitosheleza kwa chakula. Kupitia mikopo nafuu kwa wakulima, waongezaji thamani, na watoa huduma wa mnyororo wa thamani wa kilimo, benki hiyo inachochea maendeleo ya kilimo cha kisasa, chenye tija na manufaa ya kibiashara.

“Benki yetu inaamini kuwa uwekezaji katika kilimo sio tu kuhusu chakula, bali pia ni uwekezaji katika afya ya jamii, ukuaji wa uchumi na mustakabali wa taifa. Hatuwezi kuwa na taifa lenye nguvu bila kuwa na mifumo imara ya chakula bora na salama,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya TADB kwa vyombo vya habari.

TADB pia imeeleza kuwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, itaendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa chakula chenye lishe, salama, na chenye kuleta ustawi kwa Watanzania wote – si tu kwa kizazi cha sasa, bali pia kwa vizazi vijavyo.

Wiki ya Chakula Duniani ni jukwaa muhimu linalowakutanisha wadau wa sekta ya kilimo, afya, lishe, na maendeleo ya jamii kwa ujumla, kujadili changamoto na fursa zilizopo katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata chakula bora, cha kutosha na chenye lishe.






0/Post a Comment/Comments