DKT. KALEMANI AMPIGIA CHAPUO MGOMBEA UBUNGE CHATO KUSINI


Katikati ni mgombea wa Ubunge Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula

..................

CHATO

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani, amewaangukia wananchi wa kijiji cha Kakeneno kata ya Nyarutembo akiwasihi kumuunga mkono mgombea wa Ubunge Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula, kwa madai ni hazina ya maendeleo iliyokuwa inasubiri muda kutimia.

Mbali na hilo,amewaomba wananchi hao kumpigia kura nyingi mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili aweze kuongoza nchi kwa miaka mingine mitano kutokana na mafanikio makubwa ya miradi ya maendeleo aliyoitekeleza baada ya kukabidhiwa nchi mwaka 2021.

Ni baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli,aliyefariki Dunia kutokana na maradhi ya moyo.

"Namuombea kura nyingi sana mgombea Urais wa CCM, kutokana na kazi kubwa na nyingi alizozifanya baada ya kukabidhiwa nchi hii, kwa sisi wana Jimbo la Chato Kusini tunayo mengi sana ya kujivunia kutokana na uongozi wake",

"Vile vile nimuombee kura nyingi sana mdogo wangu ambaye ni mgombea Ubunge wa Jimbo hili, Paschal Lutandula,niwahakikishie mmepata jembe kweli kweli, ninamfahamu vizuri na amenisaidia mambo mengi sana katika uongozi wangu wa Ubunge kwa kipindi cha miaka 10",

"Ninatambua yapo baadhi ya mambo ambayo sikufanikiwa kuyafanya katika uongozi wangu,lakini niwahakikishie tena kuwa makablasha yote ya miradi ambayo ilikwama nimesha mkabidhi mgombea wenu ili akiapishwa tu aanze kuuashughulikia" amesema Dkt. Kalemani.

Hata hivyo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, Nichoraus Kasendamila, amesema iwapo watanzania wanatamani maendeleo hawana budi kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi kuanzia Rais, Wabunge na Madiwani.

"Ukiona watu tunajivunia amani iliyopo nchini kwetu ni muhimu utambue kuwa ni kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wetu wa CCM kuanzia Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na wengine, kwahiyo usione vyaelea lazima ujue vimeundwa, amani hiyo inatokana na sera nzuri za CCM pekee" amesema Kasendamila.

Akiomba kura kwa wananchi hao, mgombea wa Jimbo hilo, Paschal Lutandula, amewahakikishia kuwa atakuwa suruhisho la changamoto za jamii iwapo watamchagua kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.

Amesema changamoto za kata ya Nyarutembo anazifahamu vizuri ikiwemo ukosefu wa barabara ya kutoka Kakeneno hadi Mhororo, pamoja na Ile ya kwenda Kasozibakaya kuelekea makao makuu ya wilaya ya Chato.

Pamoja na mambo mengine amesema suruhisho la changamoto hizo ni kununua mitambo wa kuchonga barabara kupitia mfuko wa Jimbo huku akiahidi ndani ya siku 100 za uongozi wake atakamilisha ujenzi wa nyumba ya mganga wa zahanati ya Kakeneno.

                         Mwisho.


0/Post a Comment/Comments