Uongozi wa mgodi wa kuchimba madini ya dhahabu wa Geita Gold Mine uliopo mkoani Geita umeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwapatia huduma nzuri za kodi ambazo zimerahisisha biashara zao.
Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 10, 2025 na Meneja Mwandamizi wa kodi na msuluhushi wa migogoro ya kikodi Bw. Godvictor Lyimo wakati wa ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda na uongozi wa TRA mgodini hapo.
Amesema kupitia mifumo rafiki ya ukusanyaji wa kodi na matumizi ya teknolojia wameweza kuwa wakilipa kodi kwa hiari na kwa wakati hali ambayo imewaongezea uhuru katika utekelezaji wa majukumu yao ya uchimbaji wa madini.
Amesema mgodi huo umekuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa kufuatia kuongezeka kwa bei ya dhahabu kila siku huku akiweka wazi kuwa wanafanya kazi na wazawa kwa asilimia 94 ambao nao ni walipakodi.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda ameupongeza uongozi wa mgodi huo wa GGM kwa kulipa kodi kwa wakati na kwa hiari na kueleza kuwa wanathamini mchango wao ndiyo maana wameamua kuwatembelea na kuwasikiliza.
Amesema TRA anathamini kodi inayolipwa na Walipakodi wote nchini maana ndiyo imekuwa ikisaidia kutekeleza miradi ya maendeleo ndiyo maana wamekuwa wakifanya kila juhudu katika kuwezesha biashara na kuwasikiliza walipakodi huku wakitatua changamoto zao.
"Matokeo ya kodi yapo wazi katika maeneo yote nchini, zipo shule zimejengwa, madawati yamenunuliwa, huduma za afya zimeboreshwa, miradi ya maji imejengwa na miundombinu. Mtakubaliana nami kwamba madini yanaisha hivyo fedha za kodi zinazopatikana zinatakiwa kutumika vizuri kwa kutekeleza miradi inayoonekana" Mwenda.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa kuzingatia maadili na miongozo inayotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan.
= = = = = = =





Post a Comment