Mgombea Ubunge wa (CCM) Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula(wa kwanza kulia) akiwa na waliokuwa watia nia ya Ubunge wa Jimbo hilo.
....................
CHATO
JINA la aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chato mkoani Geita kwa kipindi cha miaka 20 na Rais wa Tanzania wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, limezidi kutajwa katika kampeni za Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini kutokana na umahiri wake wa kusikiliza na kutatua kero za watu hasa maskini.
Kutajwa kwa jina hilo ni ishara ya utumishi uliotukuka kwa kiongozi huyo ambapo baadhi ya waliokuwa watia nia ndani ya CCM wamemtaka mgombea wa nafasi hiyo, Paschal Lutandula, kuyaishi matendo ya kiongozi huyo ili kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka na kutatua kero zinazowakabili.
Akiwa kwenye mikutano ya kampeni za CCM zilizofanyika kwenye kata ya Bwanga, aliyekuwa mtia nia wa nafasi hiyo, Silvester Mapinda, amewakata wananchi kumpigia kura nyingi mgombea wa CCM ili aweze kuziba pengo la Hayati Dkt. Magufuli katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Kadhalika amemtaka mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, kuwa msikivu kwa wananchi kama alivyokuwa Hayati Dkt. Magufuli, kwa madai ndiyo ilikuwa siri ya kuaminiwa na wananchi kwa miaka 20 ya kuwaongoza katika Jimbo la Chato kabla ya kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015.
Kwa upande wake, aliyekuwa mtia nia wa nafasi hiyo, Malale Sende, amewataka watanzania kuendelea kumuamini mgombea wa Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpigia kura nyingi kutokana na dhamira njema na watu wa Jimbo la Chato kusini.
Amesema baada ya kamati kuu ya CCM kupokea mapendekezo ya watia nia ya Ubunge kote nchini chini ya uenyekiti wa Dkt. Samia, iliwapendeza kurejesha jina la Lutandula kwenye Jimbo la Chato Kusini ili awe mfariji mkuu wa wananchi wa Jimbo hilo baada ya kifo cha Hayati Dkt. Magufuli.
"Niwaombe wananchi wa Makurugusi tuendelee kumuamini Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania ambaye kwa sasa ni mgombea wa urais kupitia CCM, huyu mama anadhamira njema sana na sisi wananchi wa Jimbo la Chato Kusini ndiyo maana akamteua Lutandula kuwa mfariji wetu mkuu baada ya kuondokewa na mpendwa wetu aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. Magufuli" amesema Sende.
Hata hivyo, mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, amewaomba wananchi kuwapigia kura wagombea wa CCM akiwemo Rais Samia, Mbunge na Diwani wa kata ya Bwanga ili waweze kulitumikia taifa na kuendeleza mema yote yanayogusa maisha ya wananchi.
"Mimi Paschal Lutandula ni mtoto wenu, kwa heshima kubwa ninaomba Oktoba 29 mwaka huu mkanipigie kura nyingi ili niweze kushinda kuwa Mbunge wenu, ninayo nia njema sana kwenu baba na mama zangu wa kijiji cha Bukiriguru kata ya Bwanga, niwahakikishie hamtajuta kunichagua maana baadhi ya kero zenu zinakwenda kuwa historia ndani ya siku 100 za Ubunge wangu" amesema.
"Nia yangu kubwa ni kuwaleteeni maendeleo ya kweli, sifurahishwi na matatizo ya ukosefu wa umeme,elimu,afya na ubovu wa miundo mbinu ya barabara, ndiyo maana nimesema baada ya mimi kuapishwa kama Mbunge, nitatumia fedha za mfuko wa Jimbo kununua mtambo wa kuchonga barabara zetu za jimbo zima na mtambo huo utaanzi hapa kwenu",
"Mimi nitakuwa Mbunge msikivu na mnyenyekevu kwenu, natamani wananchi mpate fursa nyingi za kufanya kazi za maendeleo na kuinua uchumi wenu ili baada ya kazi mle bata, ndiyo maana kauli mbiu yangu ni kazi na bata, nitawapigania vijana na wanawake kupata mikopo ya aslimia 10 ili nanyi mnufaike kama wengine" amesema Lutandula.
Jimbo la Chato Kusini ni miongoni mwa majimbo nane mapya yaliyogawanya na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) kwa lengo la kusogeza karibu zaidi huduma za kibunge kwa wananchi.
Mwisho.




Post a Comment