TRA YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA NA WAFANYABIASHARA KAHAMA

:::::::
 Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umeadhimisha wiki ya huduma kwa wateja na wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wa Madini wanaoendesha shughuli zao katika soko la Madini la wilayani Kahama mkoani Shinyanga na kuwapongeza kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari. 

Akizungumza katika maadimisho hayo wilayani Kahama Oktoba 09.2015 Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema uongozi wa TRA umeamua kutembelea na kuadhimisha wiki hiyo katika soko la madini ikiwa ni kutambua mchango wao mkubwa wanaoutoa kwenye makusanyo ya kodi.

Amesema TRA inawajali walipakodi wote wakiwemo wa sekta ya madini ndiyo maana imeanzisha dawati la kuwezesha biashara ambalo miongoni mwa biashara zinazostahili kuwezeshwa ni biashara ya madini ndiyo maana amefanya ziara mgodini na pia kukutana na wachimba madini wadogo.

Amesema ili watu wauze madini vizuri kunatakiwa kuwa hakuna magendo hivyo juhudi zinafanyika ili kuhakikisha kuwa hakuna magendo hali itakayowezesha kuwepo kwa mauzo makubwa ya madini sokoni.

"Tunawashukuru sana kwa kuendelea kutuamini na kulipa kodi kwa hiari, tunawathamini sana ndiyo maana mara kwa mara tumekuwa tukiwatembelea na kuwasikiliza" amesema Bw. Mwenda. 

"Mhe. Rais anathamini sana sekta ya madini ndiyo maana ameirasimisha, na Rais aliunda Tume maalum ya kufanya maboresho ya Kodi, naamini waliwasikiliza, tunasubiri miongozo itakayotolewa tutaisimamia" amesema Kamishna Mkuu Mwenda. 

Amesema kuwa wataendelea kutekeleza miongozo wanayopewa na Rais katika kuwahudumia walipakodi kwa kutenda Haki, kujenga urafiki na Walipakodi, kutokuwaonea wala kuwapendelea walipakodi, kukuza biashara na kutoa huduma bora.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko la Madini Bw. Abel Lubasha amemshukuru Kamishna Mkuu Mwenda kwa kuwatembelea na kuwasikiliza na kueleza kuwa huduma za kodi kwa upande wao zimeboreshwa na kurahisishwa.

Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa kodi Kahama Bw. Charles Machali amesema katika siku za karibuni kumekuwa na utulivu katika kulipa kodi na kuwapongeza TRA kwa kuendelea kuwajali.




= = = = = = =


0/Post a Comment/Comments