TTCL YAHAKIKISHIA HUDUMA BORA KWA WATANZANIA WOTE



 ::::::::::::

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema litaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa, kuboresha mifumo yao, na kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania wote popote walipo ili kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na maendeleo ya mawasiliano nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Bi. Anita Moshi, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025 iliofanyika  mapema  leo Oktoba 6, jijini Dar es Salaam.

Bi Moshi  Alisema maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini utoaji wa huduma kwa wateja na kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya shirika na wananchi.

 alieleza kuwa ujenzi wa minara 1,400 ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini unaendelea kwa kasi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za mawasiliano bila kikwazo, hasa katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na changamoto za upatikanaji wa huduma hizo.

Sambamba na hilo shirika  linaendelea kutekeleza mpango wa upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi kufikia wilaya zote za Tanzania.

 Mpango huo ni msingi wa kuhakikisha huduma za intaneti na mawasiliano ya sauti zinaimarika hadi ngazi ya jamii.

Kupitia huduma ya “Faiba Mlangoni Kwako,” TTCL inaleta huduma ya intaneti yenye kasi, uhakika na viwango vya kimataifa kwa Watanzania mijini na vijijini. Bi. Moshi alisema huduma hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali, elimu mtandaoni, na huduma za kijamii.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu “Mission: Possible,” ambayo inalenga kuhimiza ubunifu, mshikamano na utayari wa kutatua changamoto katika kutoa huduma bora kwa wateja. Bi. Moshi alisisitiza kuwa kila mfanyakazi wa TTCL ni sehemu ya suluhisho na mafanikio ya shirika.

Aidha, amewasihi wateja  kuendelee kutumia vituo vya huduma kwa wateja vinavyopatikana saa 24, pamoja na maduka ya TTCL na mitandao ya kijamii kwa ajili ya kupata huduma na kutoa mrejesho. Alisema shirika linasikiliza na kufanyia kazi maoni ya wateja ili kuendelea kuboresha huduma zake.

Akihitimisha, Bi. Moshi alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuiamini TTCL na kushiriki kikamilifu katika Wiki ya Huduma kwa Wateja. Alitangaza rasmi uzinduzi wa wiki hiyo kwa mwaka 2025 na kusisitiza kuwa shirika litaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi katika safari ya kujenga taifa la kidijitali.











                                        

                              PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY TORCHMEDIA 

0/Post a Comment/Comments