Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Muungano wa Asasi za Wanawake na Watetezi wa Usawa wa Kijinsia nchini umeendelea kusisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, sambamba na kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwanzilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Mwalimu, alisema ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kisiasa ni msingi wa demokrasia jumuishi na maendeleo endelevu ya taifa.
Bi. Mwalimu alisema licha ya hatua nzuri zilizopigwa nchini katika eneo la usawa wa kijinsia, bado wanawake wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutopewa nafasi sawa katika medani za kisiasa, hasa kwenye vyombo vya habari na majukwaa ya mijadala ya kitaifa.
“Asasi zetu zinaona haja ya vyombo vya habari kuandaa midahalo, vipindi na makala maalum vitakavyowapa wagombea wanawake nafasi ya kueleza dira na sera zao. Hii itasaidia kuondoa fikra potofu kwamba siasa ni kwa ajili ya wanaume pekee,” alisema.
Aidha, muungano huo umetoa wito kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanakuwa salama, huru na jumuishi kwa wagombea wote bila kujali jinsia, huku ukikemea vikali vitendo vya vitisho na udhalilishaji wa kijinsia.
Bi. Mwalimu alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa barani Afrika baada ya kumpata Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza na kusimamia mageuzi ya kiuchumi na kijamii yenye kugusa maisha ya wananchi wengi.
Aliongeza kuwa mwaka huu umeandika historia kwa idadi kubwa ya wanawake kugombea nafasi ya urais na nyingine za juu, akiwataja Saumu Rashid wa UDP na Mwajuma Mirambo wa UMD miongoni mwa wagombea wanaoonyesha kwamba wanawake wako tayari kushika hatamu za uongozi.
“Asasi hizi zinawahimiza wanawake wote kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura, kwani kufanya hivyo ni kuchangia mustakabali wa taifa na kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika katika maamuzi ya nchi,” alisema Bi. Mwalimu.
Pia alitoa rai kwa jamii kutambua kuwa uongozi bora hauna jinsia, bali unategemea maadili, uadilifu na uwezo wa kusimamia maendeleo ya wananchi kwa usawa. “Tunahitaji viongozi wenye dira, si wa kuhukumiwa kwa jinsia bali kwa matendo,” aliongeza.
Kwa upande mwingine, Bi. Mwalimu alizitaka taasisi za habari nchini kushirikiana na asasi za kiraia katika kampeni za kuhamasisha ushiriki wa wanawake, akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni nguzo kuu ya ustawi wa taifa na mafanikio ya demokrasia ya Tanzania.















Post a Comment