CHATO
WANANCHI wa kijiji cha Bukiriguru kata ya Bwanga wilayani Chato mkoani Geita wameonyesha kufurahishwa na sera za mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula, baada ya kuahidi kuezeka jengo la zahanati ya kijiji hicho, kisha kushangiliwa na umati wa wananchi waliojitokeza kumsikiliza.
Jengo hilo linadaiwa kukwama kukamilika kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita,huku wananchi hao wakilazimika kutumia gharama kubwa kwenda kutibiwa kwenye Hospitali ya Bwanga.
Baada ya mgombea huyo kupokea kero kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye Kijiji hicho, akalazimika kwenda kujionea kwa macho yake kisha kutoa majibu yenye matumaini kwa wakazi hao ambao walidai hawajui hatma ya afya zao kutokana na kutokamilika kwa Zahanati hiyo.
"Ndugu zangu naomba mniamini kwa kunipigia kura nyingi siku ya Oktoba 29 mwaka huu,pamoja na mgombea wa Urais kupitia CCM, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na diwani wa kata hii Sanane Chai, nawahakikishia baada ya kuapishwa na ndani ya siku 100 za Ubunge wangu jengo hili litakuwa limeezekwa lote",
"Pia ndani ya mwaka mmoja wa Ubunge wangu, Zahanati yenu itakuwa imeanza kazi, ni kwa sababu kero yenu hapa ninaijua muda mrefu ndiyo maana nikalazimika kuomba nafasi hii ili nipambane kuondoa kero zenu" amesema Lutandula.
Mbali na hilo, ameahidi kuchimna Lambo la kunyweshea maji mifugo kwa gharama zake ili kupunguza kero ya migogoro ya wakulima na wafugaji na kwamba maendeleo hayawezekani iwapo wananchi wa Jimbo hilo wataendekeza migogoro hiyo.
Kadhalika ameahidi kuanzisha shamba kubwa la majani ya mifugo kwenye eneo la Chuo cha Bukiriguru kilichopo eneo hilo kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata malisho ya uhakika badala ya kutembeza ovyo mifugo yao.
"Mtakapo nichagua kuwa Mbunge wenu nitakwenda kufuatilia kwa ukaribu zaidi ili kujua sababu za kudhorota kwa Chuo chetu cha ustawishaji wa mifugo cha Bukiriguru,kwani zamani kilikuwa na umahili mkubwa wa kuhudumia wananchi wa wilaya nzima ya Chato na watu tulikuwa tukinywa maziwa bora kila siku" amesema Lutandula.
Mgombea udiwani wa Kata ya Bwera, Josephat Manyenye, akatumia fursa hiyo kumwombea kura Rais Samia, Mbunge pamoja na diwani wa kata hiyo ili washirikiane kuchochea maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Chato kusini.
"Wananchi chonde chonde ninawasihi msifanye makosa katika kuchagua viongozi bora ifikapo Oktoba 29, mwaka huu, maana viongozi wenye kuleta maendeleo kwa nchi,Jimbo na kata hii wanatokana na CCM pekee" amesema Manyenye.
Mwisho.




Post a Comment