DKT JUMA HOMERA AWASILI JIMBONI KWAKE,AWATAKA WANANCHI KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO


................

Na Mwandishi wetu- Namtumbo

WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt Juma Homera,amewataka wananchi wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,kuhakikisha wanadumisha amani,umoja na utulivu kama nguzo muhimu kwa maendeleo yao,Wilaya ya Namtumbo na Taifa kwa ujumla.

Dkt Homera amesema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Lumecha na Litola wakati wa ziara yake ya siku mbili Wilayani Namtumbo.

Amesema,wananchi wa Wilaya ya Namtumbo ni wachapakazi hivyo amewaonya kuepuka uchochezi,vurugu na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwani matumizi mabaya ya mitandao inaweza kuathiri usalama,umoja na mshikamano uliopo katika nchi yetu.

Badala yake,amewasisitiza kuwa wazalendo,kudumisha umoja na mshikamano na kuheshimu sheria za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amewaomba,kuepuka kushiriki kwenye mambo yanayokwenda kinyume na misingi ya umoja wetu ikiwemo vurugu jambo linaloweza kuharibu mustakabali wa maisha yao kwa kuwa vurugu na uvunjifu wa amani havina manufaa kwao.

“Ndugu zangu ninachotaka kuwaambia,watu wanaoshawishi nyinyi kushiriki kwenye maandamano na uvunjifu wa amani wako Ulaya wanalipwa fedha nyingi”alisema Homera.

Katika hatua nyingine Waziri Dkt Homera,amewahakikishia Watanzania kwamba mchakato kwa ajili ya kupata Katiba mpya upo mbioni,hivyo amewataka kuwa watulivu wakati huu ambao serikali itaendelea na mchakato huo.

“Nawaomba watanzania wenzengu tuwe watulivu na kuiamini Serikali yenu ya awamu ya sita kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya,mimi na wenzangu ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha nchi yetu inakwenda kupata Katiba mpya kupitia awamu hii ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan”alisema Homera.

Amesema,wakati wananchi wanadai haki basi ni vyema wao wakatimiza wajibu kwa kudumisha amani na utulivu uliopo badala ya kuwa sehemu ya vurugu na uvunjifu wa amani iliyopo.

Amewasisitiza wananchi wa Namtumbo, kuongeza juhudi ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili waweze kunufaika na uwepo wa makampuni mengi yaliyoonyesha nia ya kununua mazao hasa Tumbaku katika msimu wa kilimo 2025/2026.

Homera ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo amesema,ajenda kubwa ya Wilaya hiyo ni kilimo,na katika kufanikisha ajenda hiyo atahakikisha wakulima kupitia vikundi vitakavyoundwa wanakuwa na ekari tano huku gharama za kuandaa mashamba hayo anatoa yeye kama sehemu ya mchango wake.

“tunataka watu wetu wajikwamua na umaskini kupitia shughuli zao za kilimo,kila kijiji na kata kutakuwa na shamba ambalo wakulima wenyewe wataamua wapande zao gani la biashara”alisisitiza Homera.

Waziri Homera,amewaomba wazawa wa Wilaya hiyo wakiwemo watumishi waliopo nje ya Namtumbo kuungana na pamoja na kuwasaidia viongozi wa Serikali kwa kudumisha umoja na mshikamano ili kwa pamoja waweze kuijenga Wilaya yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya amewataka wananchi wa Namtumbo kuendelea kufanya kazi za kiuchumi ikiwemo kilimo na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwagawa Watanzania.

Amesema,amani na utulivu tulionao ndiyo msingi wa uzalishaji mali na ufanisi wa shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi,kwa hiyo ni muhimu kwa wananchi kuhakikisha wanalinda amani na mshikamano tulionao



0/Post a Comment/Comments