JUBILATION YAPONGEZWA KWA KUENDELEZA VIPAJI NA UBORA WA ELIMU


Wahitimu wa  darasa la awali (Pre-unit) ya Shule ya Awali na Msingi Jubilation wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi  Mkufunzi wa elimu ya fedha na Msimamizi wa Vijana kutoka Benki ya NBC, Bw. Yoab Ndanzi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Jubilation, Bw. Japhet Bisama wakati wakikata keki  katika mahafali ya sita yaliyofanyika leo Novemba 29, 2025, Dar es Salaam.

Mgeni Rasmi  wa Mahafali ya sita ya wanafunzi wa darasa la awali (Pre-unit) ya Shule ya Awali na Msingi Jubilation, Mkufunzi wa elimu ya fedha na Msimamizi wa Vijana kutoka Benki ya NBC, Bw. Yoab Ndanzi akizungumza jambo.

Meneja wa Shule ya Awali na Msingi Jubilation Mchungaji Dkt. Ernest Kaduna akizungumza jambo katika mahafali ya sita yaliyofanyika leo Novemba 29, 2025, Bunju, Dar es Salaam.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Jubilation, Bw. Japhet Bisama, akizungumza jambo katika mahafali ya sita yaliyofanyika leo Novemba 29, 2025, Bunju, Dar es Salaam.

Msimamizi wa Elimu Wilaya ya Kinondoni, Bi. Ngaile Lubanza akizungumza jambo katika mahafali ya sita yaliyofanyika leo Novemba 29, 2025, Bunju, Dar es Salaam.

..........

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Wazazi na walezi wametakiwa kuzingatia malezi bora kwa watoto na kuhakikisha wanapata elimu yenye ubora ambayo itawasaidia katika maisha yao, ikiwemo kuibua na kukuza vipaji vyao.

Akizungumza leo Novemba 29, 2025, katika Mahafali ya Sita ya wanafunzi wa darasa la awali (Pre-unit) ya Shule ya Awali na Msingi Jubilation iliyopo Bunju, Dar es Salaam, Mgeni Rasmi wa Mahafali hayo, Mkufunzi wa elimu ya fedha na Msimamizi wa Vijana kutoka Benki ya NBC, Bw. Yoab Ndanzi, amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuwa karibu na watoto ili kuwawezesha kupiga hatua katika elimu.

Bw. Ndanzi amesema kuwa watoto huzaliwa na vipawa mbalimbali, hivyo ni wajibu wa wazazi kuwafuatilia kwa ukaribu ili kubaini na kukuza vipawa hivyo.

“Watoto wa sasa wana vipaji vingi na wanataka kufikia malengo. Unapaswa kumsoma mtoto wako kwani wakati umebadilika; tujitahidi kuwaleta kulingana na walivyoumbwa,” amesema.

Ameipongeza menejimenti ya shule kwa kushughulikia masuala ya elimu kwa ufanisi, hususan utoaji wa programu mbalimbali ikiwemo za Teknolojia, ambazo zimewasaidia wanafunzi kuongeza uelewa.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Jubilation, Bw. Japhet Bisama, amesema kuwa shule inatoa mafunzo bora yanayozingatia maadili pamoja na programu za malezi.

Amesema kuwa wanafunzi hunufaika na masomo ya vitendo, ikiwemo michezo kama mpira wa miguu na mpira wa pete. Pia amewataka wazazi kushirikiana na walimu kwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao.

Naye Msimamizi wa Elimu Wilaya ya Kinondoni, Bi. Ngaile Lubanza, ameisifia shule hiyo kwa juhudi zake katika kuibua na kukuza vipaji vya watoto.

Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakijikita zaidi kwenye matumizi ya mitandao na kutafuta fedha, hivyo kuacha jukumu la malezi kwa walimu.

Amewataka wazazi kushirikiana na walimu na kuongeza uwekezaji katika malezi ili kuongeza tija kwa watoto.

Akizungumzia ubora wa elimu shuleni hapo, Bi. Lubanza ameipongeza menejimenti kwa uwekezaji unaoendelea ambao unaendelea kuleta manufaa kwa jamii.

0/Post a Comment/Comments