MRADI WA TRILIONI 1.57 KUCHOCHEA MAGEUZI YA KILIMO KILWA


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akimkabidhi hati isiyo asili Mwekezaji kutoka kampuni ya Pan Tanzania Agriculture Developments Ltd, Dior Feng jijini Dar es Salaam leo Novemba 29, 2025 kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo Biashara Mkoani Lindi katika wilaya ya Kilwa kwenye vijiji Vinne vya wilaya hiyo.

:::::::::::

Serikali imekabidhi ardhi kwa kampuni ya Pan Tanzania Agriculture Developments Ltd kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kilimo na viwanda wenye thamani ya Sh trilioni 1.57 katika Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.

Makabidhiano hayo yanahusisha mashamba ya vijiji vya Mavuji, Migeregere, Nainokwe na Liwiti, ambavyo vimetengwa mahsusi kwa uendelezaji wa miundombinu ya kisasa ya uzalishaji na usindikaji wa mazao katika ukanda huo wa Kilwa.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema mradi huo unatekelezwa katika zaidi ya ekari 62,000 na unatarajiwa kuzalisha ajira 300,000 ndani ya miaka 10, huku viwanda zaidi ya 80 vikitarajiwa kujengwa katika eneo maalumu la EPZ.

Alisema kilimo cha mihogo na mazao mengineyo kitaendana na ujenzi wa viwanda 150 vya kuongeza thamani ya mazao, hatua inayotarajiwa kuongeza mauzo ya nje na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani wa bidhaa za kilimo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohammed Nyundo, aliwahimiza wawekezaji wengine kuja Kilwa kwa kuwa eneo hilo lina ardhi kubwa na rasilimali nyingi, akibainisha kuwa viongozi wa mkoa na vijiji wameonyesha utayari mkubwa wa kushirikiana ili mradi huo uanze mara moja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TISEZA, Gilead Teri, alisema serikali itaweka mkataba maalum na mwekezaji ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa wakati, akibainisha kuwa kama masharti yatashindwa kutekelezwa ardhi itarejeshwa serikalini kwa ajili ya kutafutiwa mwekezaji mwingine.

Viongozi wa vijiji, akiwamo Mwenyekiti wa Mavuji, Yusuph Mohammed, walitoa wito kwa serikali kufuatilia utekelezaji wa karibu, wakisema wananchi wa eneo hilo wanatarajia ajira na huduma bora baada ya miaka mingi ya kusubiri miradi ya maendeleo.

Mwekezaji Mkuu wa Pan Tanzania, Dior Feng, alisema uwekezaji wa kampuni yake wa dola milioni 640 utaanza mara moja na utatumia teknolojia za kisasa za umwagiliaji, GPS, ndege zisizo na rubani na mifumo ya usimamizi wa mashamba, huku ukinufaisha zaidi ya wakulima 10,000 watakaounganishwa katika mnyororo wa thamani.


Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri.




0/Post a Comment/Comments