::::::::
Serikali imeweka wazi msimamo wake wa kuendeleza mageuzi katika sekta ya uchukuzi, hatua inayoiweka Tanzania katika nafasi ya juu barani Afrika kwa maendeleo ya barabara na mifumo ya usafiri wa ardhi. Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya usafiri endelevu duniani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Maseke Mabiki, alisema maboresho ya miundombinu yanatekelezwa ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo, sambamba na kufungua fursa mpya za kiuchumi. Alibainisha kuwa hatua hizo ni sehemu ya mpango mpana wa nchi kupunguza gharama na muda wa safari.
Mabiki alieleza kuwa miji mikubwa inaendelea kutayarishwa kwa mifumo mipya ya usafiri, ikiwemo ujenzi wa reli za mijini. Mpango huo utaanza Dodoma kabla ya kusambaa katika mikoa mingine ili kuondoa msongamano na kupunguza utegemezi wa magari binafsi.
Aidha, alisema wizara inaendelea kuboresha mifumo ya usafiri wa bodaboda kwa kutoa elimu na mafunzo kwa waendesha vyombo hivyo. Lengo ni kuongeza utii wa sheria, kupunguza ajali na kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na bora.
Akitaja changamoto zilizopo, Mabiki alisema miji yenye msongamano mkubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Arusha inahitaji kupanuliwa kwa barabara na kuimarisha matumizi ya usafiri wa umma. Alisisitiza kuwa kupunguza idadi ya magari binafsi mijini kunahitaji ushirikiano wa serikali, watoa huduma na wananchi.
Kwa upande wa vijijini, alisema bado kuna upungufu wa vyombo vya usafiri vinavyokidhi viwango na kwamba watoa huduma wanapaswa kuheshimu sheria zilizowekwa ili wananchi wapate huduma salama bila ubaguzi.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo,
Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, alisema kanuni mpya za usimamizi wa vyombo vya kukodi zimewapa vijana fursa kupitia vyama vya ushirika kuwa mawakala wa LATRA. Mfumo huo unaendelea kutumika katika mikoa kadhaa na umewezesha makundi ya vijana kujiendesha kiuchumi kwa kupata asilimia 20 ya makusanyo.
Suluo aliongeza kuwa serikali inaendelea kupanua ukaguzi wa kisayansi na kutafiti njia za kuanzisha huduma bora zaidi mijini, ikiwemo magari yanayotumia gesi na mifumo ya kisasa itakayomruhusu abiria kufanya kazi wakiwa safarini, kama ilivyo kwenye huduma za BRT na mataifa jirani.









Post a Comment